Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watumishi wa Tanesco waendelea kusota mahabusu

Watumishi Tanesco Pic Watumishi wa Tanesco waendelea kusota mahabusu

Fri, 25 Aug 2023 Chanzo: mwanachidigital

Fundi Mchundo wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoni Mwanza, Abdukadri Lwassa (39) na Ofisa Bohari wa Tanesco (mtunza stoo), Respicius Rwegoshora (33) wanaendelea kusota mahabusu baada ya upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi namba 5/2023 inayowakabili kutokamilika.

Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza kwa mara ya kwanza Julai 27, mwaka huu wakikabiliwa na mashtaka 125 likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya Sh2 bilioni na kuendesha genge la uhalifu.

Mashtaka mengine ni kughushi nyaraka, ubadhirifu wa mali ya Umma na kutoa nyaraka za uwongo kinyume na Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2022 Sura namba 200, wakidaiwa kutenda makosa hayo katika Ofisi za Bohari ya Tanesco iliyoko Nyakato jijini Mwanza kati ya Novemba 16, 2021 na Disemba 17,2022.

Taarifa hiyo imewasilishwa leo Alhamisi Agosti 24, 2023 mahakamani na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maxmillian Kyabona wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Kyabona amesema upelelezi wa shauri hilo unaendelea na hivyo kuiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa huku upande wa washtakiwa ukiongozwa na Wakili, Erick Mutta, Steven Kitale na Amri Linus ukiomba upelelezi huo ukamilishwe ndani ya wakati kama ilivyoelekezwa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP).

“Mheshimiwa Hakimu bado tuko ndani ya muda tunaendelea na upelelezi wa shauri hili la uhujumu uchumi hivyo niwaomba upande wa utetezi kuwa na subra tukikamilisha upelelezi hoja za awali zitaanza kusomwa,”amesema Kyabona

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Stella Kiama ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 4, mwaka huu itakapoitwa kwa ajili ya kutajwa huku washitakiwa wakirudishwa rumande.

Chanzo: mwanachidigital