Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watumishi saba wa Nida mbaroni

63228 Pic+nida

Tue, 18 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Pwani. Watumishi saba wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) nchini Tanzania wanashikiliwa na Polisi Mkoa wa Pwani kwa tuhuma za kukutwa na vitambulisho vya wananchi vipatavyo 15,000 ambavyo inadaiwa waliviiba kwa lengo la kuviuza kwa manufaa yao binafsi.

Mbali ya vitambulisho hivyo watuhumiwa hao wamekamatwa na kompyuta mpakato mbili, meza, scana, kamera, steshenari, maturubai, BVR kits, friji ndogo na vitu mbalimbali ambavyo ni mali ya Nida.

Hayo yamebainishwa leo Jumanne Juni 18, 2019 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani,  Wankyo Nyigesa  wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo amesema tukio hilo limetokea wakati wa kuhamishwa  kwa vifaa vya Nida utoka ofisi za awali maeneo ya Tanita kwenda ofisini mpya zilizoko eneo la Tamko.

Amesema watumishi  hao saba, kati yao wanaume sita, wamefanya tukio hilo wakati wakihamisha ofisi hizo kwa kuiba vitu hivyo kisha kuanza  kuviuza, kwa manufaa yao binafsi.

Kamanda huyo amesema baada ya tukio hilo uongozi wa Nida ulitoa  taarifa polisi Juni 14, 2019 kuhusiana na tukio hilo na kwamba katika kufanikisha azma yao walitumia gari ndogo aina ya Toyota Spacio yenye namba za usajili T 365 DFS ambalo pia linashikiliwa na kwaajili ya uchunguzi zaidi.

Amesema polisi walifuatilia gari hiyo iliyokuwa imebeba Jenereta mali ya Nida ambayo walikuwa wanakwenda kuiuza ambapo baada ya kupekuliwa watuhumiwa hao walikutwa na vifaa hivyo.

Pia Soma

Mbali na tukio hilo pia  jeshi hilo linawashikilia watu 29 kwa kujihusisha na matukio ya uvunjaji wa nyumba usiku na kuiba mali mbalimbali ikiwemo pikipiki moja na nguo za aina mbalimbali ambavyo vyote vinashikiliwa na jeshi hilo kwa hatua zaidi.

Chanzo: mwananchi.co.tz