Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watumishi saba kampuni ya kukusanya mapato Kinondoni kortini kwa udanganyifu

HUKUMU Watumishi saba kampuni ya kukusanya mapato Kinondoni kortini kwa udanganyifu

Wed, 7 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni, imewashitaki wafanyakazi saba wa Kampuni ya Prezidar iliyopewa jukumu la kukusanya mapato na ushuru wa masoko ya Manispaa ya Kinondoni kwa madai ya udanganyifu katika ukusanyaji na uwasilishaji wa mapato benki.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Februari 6, 2024, Mkuu wa Takukuru Kinondoni, Ismail Seleman amesema katika kipindi cha Oktoba na Novemba 2023, imefanya ufuatiliaji na uangalizi wa kichunguzi kwa muda wa siku sita na kuthibitisha kampuni hiyo inakusanya na kuwasilisha benki kiasi kidogo kuliko uhalisia wake.

Amesema kazi hiyo imefanyika kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.

"Pia tumefanya uchunguzi kuhusiana na mapato hayo na kubaini watendaji wa kampuni hiyo wamekuwa wakihujumu mapato kwa kutotumia mashine za POS ipasavyo, hivyo Januari 10, 2024 watendaji hao saba walishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni," amesema.

Amesema tuhuma hizo ni pamoja na uhujumu uchumi, ubadhirifu, kusaidia kutenda kosa, kuongoza genge la uhalifu na uchepushaji wa mapato ya ushuru na walifunguliwa kesi na. 1638/2024.

Pia imewataka wafanyabiashara wote kuzingatia miongozo inayotolewa na halmashauri na Serikali ikiwa ni pamoja na kulipa ushuru na kuhakikisha wanapatiwa stakabadhi sawa na kiasi walichotoa.

Mkuu huyo wa Takukuru amesema taasisi hiyo imeendelea kufanya programu ya Takukuru Rafiki na kutoa elimu kwa umma kupitia semina, uimarishaji wa klabu za wapinga rushwa, kufanya vipindi vya redio na televisheni na kufanya maonyesho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live