Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watumishi NHIF kizimbani kwa uhujumu uchumi

28ba40c0696d903f0f6dd43c4eb1e17e.jpeg Watumishi NHIF kizimbani kwa uhujumu uchumi

Tue, 15 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Vigogo watatu wa makao makuu ya Shirika la Taifa la Bima ya Afya (NHIF) na mmoja wa Mkoa wa Mara wamepandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Mwendesha mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wa Mkoa wa Mara, Marshal Mseja alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Stanley Mwakihaba kwamba washitakiwa watatu walisomewa mashitaka yao Novemba 23 mwaka jana na kwamba hao wameongezwa kwenye kesi hiyo.

“Lakini kati ya makosa 30 yaliyo kwenye kesi hii yanayowahusu hawa wanne ni mawili; kosa la kwanza na la 30,” alisema Mseja.

Waliopandishwa kizimbani ni pamoja na mshitakiwa wa nne, Jesca Raphael Mataba (28), Mhasibu Msaidizi wa NHIF – Musoma.

Wengine ni mshitakiwa wa tano, Grace Anthon Godi (43), Mhasibu Mkuu wa NHIF- Dar es Salaam, Anne Werema Maneno, Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa NHIF-Dar es Salaam na Myriam Angeline Fungameza (50), Ofisa Madai wa NHIF – Dar es Salaam.

Mseja aliieleza Mahakama kuwa pamoja na watu wengine ambao hawakufikishwa mahakamani jana, washitakiwa wote wanne wanahusishwa na kosa la kwanza la kuongoza genge la uhalifu lililotendwa kati ya Januari 01, 2013 na Machi 30, 2016. Katika maelezo ya kosa hilo alisema kwa nyakati tofauti na wakiwa kwenye maeneo tofauti washitakiwa hao walifanya mipango na kufuja Sh bilioni 3.870, mali ya NHIF na kuusababishia mfuko huo hasara. Washitakiwa wote waliwakilishwa na Wakili wa Kujitegemea, Ostack Mligo, ingawa kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, Hakimu Mwakihaba aliwataka kutojibu lolote mpaka kesi hiyo itakapohamishiwa kwenye Mahakama Kuu ya Kanda ya Musoma.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februali 22, mwaka huu itakapotajwa tena na washitakiwa wote walipelekwa rumande. Washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo ambao tayari walishasomewa mashitaka ni Francis Mchaki (37) aliyekuwa mhasibu msaidizi wa NHIF, Dk Leonard Mitti (51), aliyekuwa msimamizi wa NHIF na Dk Mgude Bachunya aliyekuwa meneja wa NHIF, wote walitekeleza majukumu yao Mkoa wa Mara.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live