Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watumia mtandao kilaghai walipishwa fidia mil 267.6/-

50799b02138ccde7f28df82d876a2cd1.png Watumia mtandao kilaghai walipishwa fidia mil 267.6/-

Wed, 25 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewahukumu washitakiwa wawili kulipa faini ya jumla ya Sh milioni tatu au kwenda jela miaka 2 baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya kutumia mtandao kilaghai na kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hasara ya zaidi ya Sh milioni 267.

Washitakiwa hao Baraka Mtunga na Rajabu Katunda pia wametakiwa kulipa fidia ya Sh 267,656,794.30. Mahakama pia iliagiza kutaifishwa kwa vifaa vya mawasiliano walivyokamatwa navyo zikiwemo simu mbili na kompyuta mpakato (laptop).

Hakimu Mkazi Mkuu Kassian Matembele alisoma hukumu hiyo jana baada ya makubaliano ya kumaliza kesi kwa njia ya majadiliano baina ya washitakiwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Akisoma hati ya mkubaliano Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai kuwa baada ya pande mbili kukaa na kukubaliana washitakiwa walitakiwa kulipa fidia ya Sh 267656794.30 na kwamba, tayari wamelipa Sh 200,000,000.

Simon aliieleza Mahakama kuwa makubaliano hayo pia yaliwataka washitakiwa hao wamalize kiasi kilichobaki ndani ya miezi sita.

Akisoma maelezo ya awali katika kesi hiyo wakili Simon alidai kuwa washitakiwa hao kupitia kampuni ya Uhuru One ambayo ilikuwa haijasajiliwa walitenda makosa ya kutumia na kusambaza huduma za intaneti kilaghai bila leseni.

Simon alidai kuwa, baada ya taarifa za uchunguzi kulifikia Jeshi la Polisi liliwakamata washitakiwa na walikiri kusimika vifaa vya mawsiliano na kutumia huduma za intaneti isivyo halali.

Pia alidai kuwa baada ya uchunguzi zaidi iligundulika kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo kati Desemba 13, 2019 na Septemba 28 mwaka huu.

Baada ya kusomewa maelezo hayo Hakimu Matembele aliwasomea hukumu na kuwaeleza kuwa kwa kuzingatia makubaliano waliyowekeana na DPP na kukiri kwao nafasi ya rufaa imefungwa.

"Nafasi ya rufaa inatolewa tu kwa hukumu iliyotolewa baada ya kutiwa hatiani kwa kusikilizwa ushahidi lakini kwe vile nyie mmekiri baada ya makubaliano hakuna nafasi ya dhamana,"alisema Hakimu Matembele.

Awali washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka sita likiwemo la utakatishaji fedha. Mashitaka manne yalifutwa na kusomewa hati moja ya mashitaka yenye mashitaka mawili ya kutumia mtandao kilaghai na kuisababishia TCRA hasara.

Chanzo: habarileo.co.tz