Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watuhumiwa unyang’anyi wadai kupigwa na polisi

HUKUMU Watuhumiwa unyang’anyi wadai kupigwa na polisi

Tue, 12 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Serikali ikiieleza Mahakama kuwa bado inaendelea na upelelezi katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayowakabili washtakiwa watano wakiwemo askari polisi, washtakiwa wawili kati ya hao wamedai kuwa walipigwa na Polisi walipofikishwa kituo cha Polisi Chang'ombe na kusababisha kuwa na maumivu mwili mzima.

Washtakiwa hao, ambao wanadai kupigwa na askari wakiwa kituo hapo ni mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo, Ashiraf Sango (31) ambaye ni mfanyabiashara pamoja na mshtakiwa wa tano, Emmanuel Jimmy (31) ambaye ni wakala.

Hayo yameibuka, leo Desemba 11, 2023 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Novemba 30, 2023, washtakiwa hao wawili waliunganishwa katika kesi ya jinai namba 197/2023 inayowakabili waliokuwa askari Polisi watatu na kisha kusomewa shtaka moja la unyang'anyi wa kutumia silaha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Washtakiwa hao wametoa madai yao, muda mfupi baada ya Wakili wa Serikali, Asiati Mzamiru kuieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amiri Msumi, kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Mzamiru baada ya kueleza hayo, ndipo mshtakiwa wa Sango aliponyoosha mkono juu akiashiria kuwa anataka kuzungumza na alipopewa nafasi ya kuongea alidai kuwa alivyokamatwa na kufikishwa kituo cha Polisi Chang'ombe alipigwa na polisi na kusababisha mwili wake kuwa na maumivu makali.

"Mheshimiwa hakimu, naomba maneno haya ninayoyasema uyaweke katika kumbukumbu ya Mahakama. Mimi nilipokamatwa na kufikishwa kituo cha Polisi Chang'ombe, nilipigwa sana mpaka sasa hivi mwili wangu wote una maumivu makali," amedai mshtakiwa Sango.

Sango baada ya kumaliza kuongea, naye mshtakiwa Jimmy, alidai kuwa mwili wake umekuwa na maumivu yaliyotokana na kupigwa na askari Polisi akiwa kituo cha Polisi Chang'ombe, hivyo aliiomba Mahakama kurekodi hicho alichokieleza ili kiingie kwenye kumbukumbu za Mahakama.

Hakimu Msumi baada ya kusikiliza kesi hiyo aliahirisha hadi Desemba 21, 2023 kesi hiti itakapotajwa na washtakiwa wanaendelea kubaki rumande kutokana na shtaka la unyang'anyi wa kutumia silaha linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni waliokuwa askari kanzu watatu mwenye namba F 7149 D/Coplo Ramadhani Tarimo(42) maarufu kama Rasta na mkazi wa Kipawa; G 7513 D/Coplo Majid Abdallah(35) na mkazi wa Kunduchi na WP 6582 D/ Coplo Stella Mashaka( 41) mkazi wa Railway.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, Agosti 28, 2023 katika eneo la Kurasani, karibu na ofisi za Uhamiaji, Ilala, ambapo siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja waliiba Sh 90 milioni kutoka kwa Grace Donald Matage.

Inadaiwa kabla na baada ya kufanya wizi huo, walimtishia Grace kwa bunduki ili waweze kujipatia fedha hizo bila kikwazo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live