Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watuhumiwa uhalifu 13 washikiliwa Polisi

Juma.webp Watuhumiwa uhalifu 13 washikiliwa Polisi

Wed, 6 May 2020 Chanzo: --

JESHI la Polisi mkoa wa Mwanza linawashikilia watuhumiwa 13 kwa tuhuma za kujihusisha na makosa mbalimbali yakiwamo mauaji yaliyohusisha ramli chonganishi.

Akizungumza na wanahabari Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Muliro Jumanne, alisema baada ya kufanya operesheni ya kuzuia vitendo vya uhalifu na kuwakamata baadhi ya watu wanaojihusisha na vitendo hivyo, Mei 2, mwaka huu majira ya usiku katika Kitongoji cha Imalange, Kijiji cha Mwanangwa, Wilaya ya Misungwi, alikamatwa mtuhumiwa wa kosa la mauaji, Rodha Shabani (27).

Alisema baada ya kuhojiwa mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na mauaji ya Ndebeto Kakula (78), aliyeuawa Aprili 29, mwaka huu, kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali ambacho baadaye ilibainika kuwa ni panga sehemu ya shingoni wakati akitoka kisimani kuchota maji.

Alisema tukio hilo lilitokea baada ya mganga wa kienyeji, Muhangwa Paul, kumpigia ramli chonganishi mtuhumiwa kwa madai aliwaroga watoto wake wawili na kusababisha vifo vyao.

Alisema upelelezi umewezesha kukamatwa kwa mganga huyo na panga lililotumika limepatikana, na kwamba upelelezi ili umekamilika kwa asilimia 90.

Alisema kuanzia Machi hadi Aprili mwaka huu, katika maeneo ya Jiji la Mwanza, Jeshi la Polisi liliendesha operesheni dhidi ya wahalifu wa matukio ya uvunjaji wa nyumba usiku na wizi wa vifaa vya nyumbani vya kielektroniki, ambapo katika operesheni hiyo watuhumiwa zaidi tisa walikamatwa.

Akiwataja baadhi ya watuhumiwa ni Juma Said(35), Saitoti Makokoyo (28), Kelvin Irizikiwa (32), Hussein Masoud (42), Kiroba Heka (38), Kudra Melikiadi (23), Busumbilo Charles (25 ), Simon Deonatus na Ally Bakari (24).

“Walifanikiwa kukamata flat tv 30, mota za mashine 2, deki mbili , subwoofer mbili na vifaa vya kuvunjia kama vile nyundo, shoka, nondo, simu 30 tindo, spana, plaizi, baruti na vifaa vya kulipulia, ”alisema Muliro.

Aliongeza kuwa katika tukio lingine walimkamata mama aliyetelekeza watoto kwenye mazingira hatarishi ya majaruba ya mpunga, ambapo Aprili 29 majira ya asubuhi katika eneo la Nyakato, Wilaya ya Ilemela, mwanamke huyo, Happines Mafuru (23), alikamatwa kuhusiana na tukio la kutelekeza watoto wawili Aprili 27 mwaka huu katika mashamba ya mpunga.

Chanzo: --