Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watuhumiwa 10 wapandishwa kortini kwa wizi wa shaba

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watuhumiwa 10 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kuiba shaba yenye thamani ya Sh190,000 huku wakijia kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Washtakiwa hao ni mkazi wa Tabata, Ally Athuman (29), mkazi wa Ilala Bungoni, Abdallah Otto(28), mkazi wa Tabata Bima, Donard Manyori (31) na mkazi wa Buza  Athuman Mkumbuya (32).

Wengine ni mkazi wa Kinondoni Shamba, Mkina Holela (32), mkazi wa Kigamboni, Allen Paulo (30), mkazi wa Vijibweni, Hashim Mashaka (31), mkazi wa Mbagala Kibuguni, Said Mfupa (29), mkazi wa Kiwalani, Dominic Mwaipaja (33) na mkazi wa Mbezi, Orgenes Joseph (32)

Akisoma hati ya mashtaka leo, wakili wa Serikali, Faraja Ngukahi mbele ya Hakimu Mkazi, Maila Kasonde amedai shtaka la kwanza washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa katika tarehe tofauti  Januari mwaka huu wakiwa maeneo ya Dar es Salaam waliiba mali na kusafirisha huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria. 

Katika shtaka la pili, washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa kati ya Januari 18 na 19 mwaka huu wakiwa  maeneo ya Dar es Salaam walikutwa na vifurushi sita vya madini aina ya kopa na kila  kimoja vilikutwa na vipande 38 vyenye thamani ya Sh190,000 huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Ngukabi amedai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na aliiomba Mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa wote kwa pamoja walikana makosa yanayowakabili. 

Hakimu Kasonde  aliwatajia masharti ya dhamana ambayo ni kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja anayetambulika kisheria atakayesaini bondi ya Sh10 milioni na kila mshtakiwa ametakiwa kusaini fedha taslimu Sh10 milioni au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.

Washtakiwa hao walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na wamerudishwa rumande na kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 13,2019.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz