Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu wenye mapanga wavamia mtaa Dar, wacharanga wananchi na kupora mali, fedha

PANGA Watu wenye mapanga wavamia mtaa Dar, wacharanga wananchi na kupora mali, fedha

Thu, 1 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu watano wamejeruhiwa huku mmoja akiwa mahututi baada ya kundi la vijana kuvamia mtaa wa Tagusako, Tabata jijini Dar es Salaam, kupora mali na fedha taslimu."

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mashuhuda na viongozi wa mtaa huo, walisema vijana hao wakiwa na silaha za jadi waliwakata kwa mapanga waendesha bodaboda watatu na wananchi wawili, huku wengine wakikatwa vidole.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Kata ya Tabata, Peter Joakimu, alisema tukio hilo lilitokea Agosti 28, mwaka huu, majira ya saa tano usiku na kundi hilo la vijana lililokuwa limebeba silaha kama visu na mapanga. Alisema wanamshikilia mtu mmoja ambaye alionekana na watuhumiwa hao.

"Kweli vijana hao walifanya uhalifu huo, waliwaumiza wananchi watatu pamoja na vijana wawili wa bodaboda ambao kati yao mmoja anafahamika kwa jina la Nelson Aruya (30), ambaye mpaka sasa hali yake sio nzuri amelazwa Hospitali ya Amana,” alisema Joakimu.

Mwenyekiti huyo alisema kundi hilo la wahalifu lilivamia maduka na kupora fedha na kuwanyang’anya simu za kiganjani wananchi.

"Wahalifu hao walivamia wateja waliokuwa kwenye baa ya Shooters Pub, na kuanza kuwakata mapanga kichwani na kuwakatakata viungo vya mwili wateja waliokuwapo na kuwaamuru walale chini,” alisimulia.

Alisema walishirikiana na Kituo cha Polisi Tabata na kumpata mhusika mmoja ambaye majira ya mchana siku ya tukio, alionekana na watuhumiwa wengine nyumbani kwake. Hata hivyo, alipofikishwa kituoni alibainika kuwa sio mkazi wa eneo hilo.

Mjumbe wa eneo hilo, Saida Mashine (60), alisema vijana hao walivamia eneo hilo mapema wakati baadhi ya wananchi wakiwa hawajafunga biashara zao.

"Nilikuwa nipo ndani nikasikia kelele nje nilipotoka nikamkuta kijana mmoja wa bodaboda anatoka damu nyingi kichwani na mkononi, huku akiwa anapiga kelele anakimbia ikanilazimu nifanye utaratibu apelekwe hospitali huku nikiwa nimeishikilia pikipiki yake,” alisema Mashine.

Tukio hilo alidai limeathiri uchumi wa eneo hilo baada ya kuwapora wananchi fedha na mali zilizokuwa kwenye biashara zao.

Mmoja wa majeruhi, aliyekatwa mapanga kichwani na kukatwa kidole cha mkono Abduli Salum Maketa (35), alisema vijana hao walimvamia akiwa anashusha abiria na kupora simu na fedha alizokuwa nazo.

"Nilikuwa nimesimama nasubiri abiria anilipe pesa nikaona kundi la watu linakuja nikidhani ni ulinzi shirikishi waliponikaribia wakatoa mapanga wakaniambia nitoe simu pamoja na pesa nilizokuwa nazo hapo tayari wamenipiga panga la kichwa nikawa sijitambui nikakimbizwa hospitali,” alisema Maketa.

Naye dada wa majeruhi, Sara Aruya, alisema hali ya mdogo wake sio nzuri anaendelea na matibabu Hospitali ya Amana.

"Nelson hali yake sio nzuri alikatwa mapanga mawili kichwani vile vile alikatwa kidole cha mkono ninavyokuambia hata kuongea kwake ni kwa shida, tunaomba serikali isimamie jambo hili kusudi hawa wanaofanya uhalifu huu wadhibitiwe,” alisema.

Shuhuda mwingine Sofia Hamisi, alisema alikuwa anaelekea nyumbani na kuvamiwa na vijana hao ambao walimpora simu na kutishia kumchoma kisu.

Kutokana na tukio hilo baadhi ya wananchi wamedai kuhofia kutoka nje, huku wakiliomba jeshi la polisi kuimarisha ulinzi kutokana na kuongeza kwa matukio ya uhalifu.

Kaimu Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Willium Mponda, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa askari wanawasaka waliohusika na wanawashikilia watu kadhaa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live