Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu sita wakamatwa uchochezi vita ya koo

11562 Watu+sita+pic TanzaniaWeb

Tue, 17 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tarime. Watu sita wanashikiliwa na polisi katika kituo cha Sirari wilayani hapa Mkoa wa Mara, kwa tuhuma za kula njama ya kuanzisha mapigano baina ya koo mbili za Wakira na Wanyabasi katika vijiji vya Kebweye na Kyoruba.

Kamanda wa polisi Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe alisema jana kuwa watuhumiwa walikamatwa kutokana na uchochezi wa koo wakigombea mipaka ya vijiji hivyo.

Mwaimbambe alisema ‘wachochezi’ walipanga kuanzisha vita na ilikuwa imepangwa kufanyika lakini polisi walipata taarifa kupitia vyombo vyake na kufanikiwa kuizima kabla ya haijatokea.

“Walitaka kupigana tumeingilia kati, hakuna aliyekufa wameomba vikao vya mwafaka,” alisema Mwaibambe kupitia ujumbe wake mfupi wa simu ya mkononi.

Akizungumza tukio hilo, mwenyekiti wa kijiji cha Kebweye, Marwa Nyasoko alisema vita hiyo ilizuka Julai 13 majira ya jioni kwa wananchi kutoka upande wa kijiji cha Kyoruba na kuvamia miji iliyopo mpakani na kuchoma nyumba.

“Saa tatu usiku walivamia miji mitatu ya mpakani wakachoma nyumba mbili za nyasi na kukatakata bati zilizokuwa zimeezeka nyumba moja, lakini polisi walifika mapema na kuwatawanya,” alisema Nyasoko.

Mgogoro huo wa ardhi unaelezwa kudumu kwa zaidi ya miaka 30, wananchi wanaiomba Serikali kutumia barua ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi aliyoiandika miaka ya 1980 kuutatua.

Pia, wananchi hao waliitaka Serikali kutouita mgogoro huo kuwa wa kisiasa badala yake, utatuliwe ili kuleta amani katika koo hizo mbili ambazo zinaongea lugha moja.

“Binafsi naumia sana ninapoona watu tunaoongea lugha moja tunaoana na kushiriki kwenye sherehe pamoja tunagombana, hata kwa makabila mengine tunajiabisha sana,” alisema Nyasoko.

Naye mkazi wa kijiji cha Kyoruba, Baraka Sarya aliutaka uongozi wa wazee wa mila kuingilia kati tatizo hilo kwa kuwa wao wana sauti kwa jamii, hasa wakivalia njuga suala lolote linaisha.

Pia, wananchi hao waliiomba Serikali kutumia eneo linalogombewa kuweka mradi wa jamii ili kumaliza ugomvi wa mipaka hiyo kama ilivyofanyika kwa mpaka wa Wancharya na Warenchoka.

Chanzo: mwananchi.co.tz