Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu 76 mbaroni kwa uhalifu Dar

1578ab333cbac800f3ab05019a43b69c Watu 76 mbaroni kwa uhalifu Dar

Sat, 2 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JESHI la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limewakamata watu 76 kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya kihalifu na kusababisha kero kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alisema miongoni mwa waliokamatwa wanatuhumiwa kujihusisha na wizi wa magari, unyang’anyi wa kutumia silaha na wizi wa vifaa vya magari.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limeendelea na jitihada za kuzuia uhalifu na kufanya misako mikali ya kufuatilia wahalifu mbalimbali wa makosa ya jinai. Katika misako hiyo jeshi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 76 wa makosa ya jinai ambayo ni kero kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam,” alisema.

Aliongeza, “Miongoni mwa waliokamatwa ni wanaojihusisha na wizi wa magari na vifaa vya magari, wizi wa pikipiki, ukwapuaji wa mikoba kwa kutumia pikipiki, unyang’anyi wa kutumia silaha na matukio ya uvunjaji usiku na mchana.” Alisema kati ya watuhumiwa 76 waliokamatwa, watano wanadaiwa kujihusisha na upokeaji wa vifaa vilivyoibiwa kwenye magari.

“Watuhumiwa hawa walikamatiwa maeneo tofauti ya Dar es Salaam yaliyoshamiri kwa upokeaji na uuzaji wa vifaa vya wizi vya magari hususani Kariakoo, Ilala Bungoni, Tabata na maeneo ya Mbezi Beach Mkoa wa (kipolisi) Kinondoni… Watuhumiwa walipekuliwa na kukutwa na vifaa vya magari kama power window, taa za magari mbalimbali, matairi ya magari, side mirror, air cleaner, bumper, wheel cap na zingine,” alisema.

Muliro alieleza kuwa watuhumiwa wengine 24 walikamatwa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na uchunguzi ulibaini kuwa walikuwa wakiiba vifaa vya magari na kwenda kuuza. Alisema polisi waliwakamata pia watu wengine saba kwa tuhuma za kuiba magari matatu.

Aidha alisema watuhumiwa 40 ni wa unyang’anyi wa kutumia silaha, uvunjaji wa nyumba usiku na uporaji wa mikoba kwa kutumia pikipiki.

“Kuanzia Septemba 1 hadi 30, mwaka huu tulifanya misako maeneo mbalimbali ya jiji na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao. Watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na zana mbalimbali za kufanyia uhalifu yakiwemo mapanga matatu, kamba za katani, mikasi mikubwa ya kukatia chuma, nondo za kukunjia madirisha na pikipiki mbili,” alisema.

Muliro alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola kupitia mifumo ya kisheria kuanzia mwezi Januari hadi Septemba 2021 limefanikiwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa makosa mbalimbali ya jinai na baadhi yao kupewa adhabu.

“Jumla ya kesi nane za kubaka zilifikishwa mahakamani na watuhumiwa nane walikutwa na hatia na kupewa adhabu mbalimbali. Waliopata kifungo cha maisha ni watatu, kwenda jela miaka 30 watu watatu na wengine wawili walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela. Kesi 19 za unyang’anyi wa kutumia silaha zilifikishwa mahakamani na watuhumiwa 33 walikutwa na hatia na kutupwa jela kutumikia kifungo cha miaka 30,” alisema.

Alisema kuwa kesi mbili za kuvunja nyumba usiku na mchana na kuiba zilifikishwa mahakamani ambapo watuhumiwa wanne walihukumiwa vifungo, wawili kati yao walifungwa miezi sita jela na wawili walifungwa miaka mitatu jela.

Muliro alisema kesi tano za makosa ya kulawiti zilifikishwa mahakamani na watuhumiwa watano walifungwa, wawili kati yao walifungwa mwaka mmoja na kulipa faini na watuhumiwa wawili walifungwa miaka 30, huku mtuhumiwa mmoja akifungwa kifungo cha nje na kulipa faini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz