Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu 60 wanashikiliwa na polisi kwa kuhujumu wa miundombinu Tanesco

20471 Pic+mambo+sasa TanzaniaWeb

Wed, 3 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watu 60 wamekamatwa na Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kuhujumu miundombinu ya umeme baada ya jeshi hilo kufanya operesheni kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Watuhumiwa 10 kati ya 60 wamefikishwa mahakamani kusomewa mashtaka yao, wengine 30 wanatakiwa kulipa faini Tanesco kwa kosa la kuingilia miundombinu, huku 20 wakiendelea kuhojiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari  leo, Kamanda wa Polisi kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema operesheni hiyo ni endelevu katika maeneo yote ya jiji na kuwataka wanaojihusisha na vitendo vya uhujumu wa miundombinu kuacha mara moja.

“Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na wimbi la kujiunganishia umeme moja kwa moja kwenye braketi, wizi wa mita na kuchezewa mita kwa ndani, huku wengine wakiiba umeme kupitia kwenye waya kabla ya kufika kwenye mita,” alisema Mambosasa.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo limekamata pikipiki 104 katika wilaya tatu za Temeke, Ilala na Kinondoni kwa kosa la kuingia maeneo ya mjini bila kibali.

“Pikipiki hizo hazitakiwi kuingia katikati ya mji ili kuzuia matukio ya uhalifu yaliyokithiri yanayofanyika kwa kutumia pikipiki, lengo ni kuhakikisha kunakuwa na usalama wa kutosha na utii wa sheria za usalama barabarani,” alisema.

Wakati huo huo, Kamanda Mambosasa amesema Septemba 19 jeshi hilo lilikamata silaha aina ya Short gun’ iliyokatwa kitako na mtutu.

“Silaha hiyo yenye namba 69323 ilipatikana baada ya upekuzi wa maungoni mwa mtu mmoja akiwa ameificha kwapani ndani ya shati,” amesema

Kuhusu ukamataji wa makosa ya usalama barabarani, amesema kuanzia Septemba Mosi hadi 30 jumla ya makosa yaliyopatikana ni 60,184 na zaidi ya Sh2 bilioni zimekusanywa kufuatia makosa hayo.

“Idadi ya magari yaliyokamatwa ni 45,916, pikipiki 1,820, daladala 21, 968, magari mengine(binafsi na malori) 1,980 na bodaboda waliofikishwa mahakamani kwa makosa ya kutovaa kofia ngumu na kupakia mishikaki ni 89.”

“Madereva wanatakiwa kuwa na leseni zao wakati wote kwa ajili ya ukaguzi wa magari unaoendelea. Wamiliki pamoja na watumiaji wote wanatakiwa kutii sheria za barabarani ili kupambana na ajali zinazoweza kuzuilika,” amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz