Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu 100 kutoa ushahidi kesi wizi Sh780 milioni NMB

Nmb Jengo Alilozindua Rais Kikwete Jijini Dar Es Salaam Watu 100 kutoa ushahidi kesi wizi Sh780 milioni NMB

Fri, 9 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

Serikali imesema mashahidi zaidi ya 100 wanatarajia kutoa ushahidi katika kesi ya wizi wa Sh780 milioni inayowakabili washtakiwa 14 wakiwemo walinzi wa kampuni ya ulinzi ya SGA.

Mashahidi hao wanatarajia kuanza kutoa ushahidi wao, Juni 26, 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya upelelezi wa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 41/2022 kukamilika na washtakiwa kusomewa maelezo yao.

Mbali na idadi hiyo ya mashahidi, pia vielelezo 101 vinatarajia kutolewa mahakamani hapo na mashahidi hao kwa ajili ya kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa.

Washtakiwa hao wakabiliwa na mashtaka saba yakiwemo ya wizi wa kuaminika na kutakatisha kiasi hicho cha fedha.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuiba Sh780 milioni zilizokuwa zikisafirishwa kutoka katika benki ya NMB Tawi la Mbezi Beach kwenda makao makuu ya benki (NMB House), kwa kutumia gari la kubebea fedha mali ya kampuni hiyo ya ulinzi.

Imeelezwa kuwa wakiwa njiani watuhumiwa hao wanadaiwa kuiba fedha hizo na kisha kutelekeza gari hilo likiwa halijazimwa eneo la Mbagala Rangitatu, huku likiwa na masanduku matatu ya kutunzia fedha (safe) pamoja silaha mbili aina ya shortgun Pump na Shortgun Protector zikiwa na jumla ya risasi 17.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Clara Chame akishirikiana na Slyvia Mitanto ameieleza mahakama hiyo leo Ijumaa Juni 9, 2023 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalira wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa hoja za awali (PH).

Wakili Chame amewataja washtakiwa hao kuwa ni Menjestu Mselema, Tulipo Mwakuzi, Bernard Machimbo, Joseph Mwatonoka, Juma Mbulinda, Joseph Mpondo maarufu kama Khomango, Englibert Masare, Beda Mmali, Kaisi Nasibu na Godwin Erio, wote wafanyakazi wa kampuni ya ulinzi ya SGA na wakazi wa Dar es Sakaam

Wengine ni Oswald Mselema na John Mkamba ambao ni wafanyabiashara, huku Edes Hyera na Sylidion Odilo wakiwa ni wafanyakazi wa SGA.

Kabla kuwasomea washtakiwa hao PH, wakili Chame aliwakumbusha mashtaka yao kwa kuwasomea shtaka la kwanza hadi la nane.

Hata hivyo, washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, walikubali majina yao na siku walipofikishwa mahakamani, huku wakikana kutenda makosa yao.

Hakimu Rugemalira baada ya kusikiliza shauri hilo, amepanga siku nne mfululizo kusikiliza kesi hiyo kuanzia Juni 26 hadi Juni 29, 2023

Mashtaka yao:

Shtaka la kwanza linalowakabili washtakiwa wote, inadaiwa kati ya Juni Mosi , 2020 na Juni 8, 2020 katika Jiji la Dar es Salaam walikula njama za kutenda kosa la wizi.

Shtaka la pili ni wizi, linawahusu washtakiwa wote, wanadaiwa Juni 8, 2020, katika benki ya NMB tawi la Mbezi Beach, walijipatia Sh780 milioni.

Wakili Mitanto alidai shtaki la tatu ni utakatishaji fedha na linawakabili washtakiwa, Mselema, Mwankusye, Machimbo, Mwatonoko, Mbulinda, Mponda, Masore, Mmali, Masibu, Mkamba, Hyra na Odilo, ambapo kati ya Juni 8, 2020 na Agosti 31, 2020 katika jiji la Dar es Salaam, walijipatia sehemu ya fedha hizo wakati aakijua fedha hizo ni zinatokana na kosa la tangulizi la wizi.

Shtaka la nne na la tano ni la kutakatisha fedha linalomkabili mshtakiwa Mwankusye pekee yake ambaye anadaiwa kutenda kosa hilo Julai Mosi 2018 na Mei 30, 2020 katika maeneo tofauti ya Makambako mkoani Njombe.

Siku hiyo Mwankusye, kwa lengo la kuficha uhalali wa fedha, alitumia sehemu ya Sh780 milioni kwa kununua pikipiki moja na Power Tiller, yenye thamani ya Sh33 milioni, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la wizi.

Pia shtaka la sita na saba ni la kutakatisha fedha ambalo linalomkabili Mpondo, ambaye anadaiwa kutenda kosa lake kati ya Mei 30, June 8, 2020, Julai Mosi na Septemba 2020 katika eneo la Ikungi mkoani Singida, kwa lengo la kuficha uhalali wa fedha, alitumia sehemu ya Sh780 milioni anazodaiwa kuiba kwa kununua viwanja viwili vyenye thamani ya Sh7milioni.

Shtaka la nane ni la kutakatisha fedha na linamkabili Mwatonoka, ambapo anadaiwa Mei 20, 2020 katika maeneo ya Chimala mkoani Mbeya, kwa lengo la kuficha uhalali wa fedha, alitumia sehemu ya Sh780 milioni kwa kununua magunia 910 ya mpunga yenye thamani ya Sh47.2 milioni wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la wizi.

Hata hivyo mshtakiwa Mkamba, Hyra na Odilo wapo nje kwa dhamana kutokana na kutokuwa na mashtaka ya kutakatisha fedha.

Chanzo: Mwananchi