Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto wa ibilisi walivyotikisa Tanga

Panya Road2 Watoto wa ibilisi walivyotikisa Tanga

Sun, 11 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Matukio ya wananchi kuvamiwa, bodaboda, wenye bajaji kupigwa na uporaji simu na pochi za wanawake unaofanywa na vijana wahalifu wanaojiita watoto wa ibilisi ni matukio yaliyotikisa jijini hapa kwa mwaka 2022.

Kuanzia siku ya kuukaribisha mwaka 2022 usiku wa mkesha watoto wa ibilisi walichoma moto matairi na kupiga mawe kwenye mabati ya nyumba katika mitaa mbalimbali, kulipua baruti na eneo la Magomeni walifanya vurugu kiasi cha kupambana na askari polisi waliokuwa wakiwazuia.

Licha ya baadhi yao kukamatwa na kufikishwa kituo kikuu cha polisi Chumbageni, ilikuwa kama wamechochewa kwa kuwa matukio ya uporaji na watu kujeruhiwa mitaani hasa nyakati za usiku, yaliendelea kwa kasi kubwa.

Miongoni mwa matukio yaliyoripotiwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Safia Jongo kabla ya kuhamishwa ni pamoja na kuwajeruhi maharusi waliokuwa katika tukio la kupewa zawadi mtaa wa Kisosora.

“Katika tukio hilo waliwajeruhi kwa mapanga maharusi, lakini pia wanawake waliokuwa wakisherehekea tafrija ya kumpa bibi harusi zawadi, tayari vijana watano tunawashikilia kwa tuhuma za uvamizi huo,” alisema Jongo.

Pia Mwananchi ilifahamishwa kuwa baadaye kila nyumba iliyokuwa ikifanya harusi wakati wa kucheza ngoma za usiku, vigodoro washiriki walikuwa wakichanga fedha kwa ajili ya kuwahonga watoto wa ibilisi wakivamia wasifanye uporaji au kuwadhuru.

Matukio hayo yalipungua baada ya Jongo kuingia mwenyewe mitaani usiku akiongoza kikosi maalumu alichokuwa amekiunda kuwadhibiti watoto hao wa ibilisi, lakini baadaye walirejea tena.

Matukio hayo yalisababisha vyombo vya dola na wananchi kuanza kutupiana lawama kwa kutowajibika kikamilifu kudhibiti.

Wananchi walilalamika

Miongoni mwa waliolalamika kwenye vyombo vya habari ni Mwanahamisi Ramadhani, mkazi wa Kisosora kata ya Chumbageni aliyejeruhiwa na watoto wa ibilisi, ambapo alisema kuwa waliomvamia waliachiwa na polisi na kuendelea kuzurura mitaani.

Hata hivyo, Kamanda Jongo akilifafanua hilo alisema kuwa wazazi ndio wanastahili kubeba lawama kwa sababu wanaona nyendo zao na hawawakemei wala kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola.

Alisema na hata wakikamatwa kwa kujihusisha na uhalifu wa uporani wanakwenda polisi kuwadhamini na wengine wanawatumia viongozi wa kuchaguliwa kama madiwani na wenyeviti wa Serikali za mitaa kuliomba jeshi hilo kuwaachia.

Nini kimefanyika kudhibiti

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba alisema baada ya kuhamishiwa mkoani hapa alikuta watoto wa ibilisi wameshamiri, ambapo aliamua kukutana na viogozi wa madhehebu yote ya dini, asasi za kiraia, viongozi wa Serikali za mitaa na kujadiliana nao njia ya kufanya ili kudhibiti wimbi hilo.

“Ni fedheha kwa mwanao kuitwa mtoto wa ibilisi, maana yake mzazi anatakiwa kuitwa ibilisi...tulianzia hapo tukajadili kisha tukawapa majukumu kila mzazi kutekeleza wajibu wake wa kumlea mwanaye,” alisema Mgumba.

Alisema ni jambo jema kuona kuwa hakuna tena matukio ya uhalifu unaofanywa na watoto wa ibilisi na hivi sasa amani imerejea mitaani.

“Sikupenda kuona sifa ya amani iliyopo Mkoa wa Tanga inaharibiwa na vijana hao wa ibilisi na kila atakayejihusisha atakamatwa na kuchukuliwa hatua bila kujali ni mtoto wa nani,” alisema.

Akilizungumzia hilo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Msafiri Mbilu alisema katika kipindi cha wimbi la watoto wa ibilisi walipokuwa wakifanya uhalifu makanisa yalifanya maombi, ikiwa ni pamoja na kutoa mahubiri ya kuwakumbusha wazazi wajibu wao wa kuwalea vijana kwa kumtambua Mungu.

“Mwaka 2022 haukuwa mzuri kwa eneo letu la Tanga, watoto wa ibilisi waliuvaa uibilisi na kufanya uhalifu bila kujali, lakini tulifanya maombi ili vijana waishi kwa kumtukuza na kumuogopa Mungu,” alisema Askofu Mbilu.

Naye Sheikh wa Baraza kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) mkoani hapa, Juma Luwuchu alisema watoto wa ibilisi ni matokeo ya wazazi kushindwa kutimiza wajibu wa kuwalea watoto wao kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume Mohammad (S.A.W), aliyesema kuwa kila mzazi ataulizwa siku ya kiyama aliwachungaje watoto na wake wao.

“Kila mmoja akitambua kwamba ni mchunga na atakuja ulizwa aliwachungaje walio chini ya himaya yake basi ataogopa kuwaacha watoto kufanya uhalifu hadi kujipa majina ya ibilisi,” alisema Sheikh Luwuchu.

Kwa upande wa Zainabu Ashrafu, mkazi wa Mtaa wa Mikanjuni jijini Tanga anasema pamoja na kwamba wazazi wanakosea katika malezi na namna ya kuishi na waoto wao majumbani, watumishi wa vyombo vya dola wanashindwa kushughulikia wakitafuta kisingizio kuwa wazazi wameshindwa.

“Huku Mikanjuni tumeathirika vibaya sana, watoto wa ibilisi walikuwa wakitoka mitaa ya jirani kutupora na kutunyang’anya, hasa sisi wanawake,” alisema Zainab.

“Ulifikia wakati kama unapata abiria usiku unamwambia atenge na fungu la kuwapa watoto wa ibilisi, kama wakituotea ujue siyo bahati yako, ni lazima uwape ulichonacho ndipo wakuachie, vinginevyo watanyang’anya pikipiki au wakupige,” alisema Charles Minja wa Sahare, jijini Tanga.

Naye Mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya CCM Wilaya ya Tanga, Nassor Makau alisema kuna mahali wazazi wameshindwa kutimiza majukumu ya kuwalea watoto wao.

“Ndio maana Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alipotamka kupambana na panya road na watoto wa ibilisi wakaacha uvamizi na sasa tunamaliza mwaka kwa amani, lakini utakumbukwa kwa matukio mabaya ya watoto wetu,” alisema Makau.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live