Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watendaji kata watano wapandishwa kortini

Sat, 20 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar Es Salaam. Waliokuwa maofisa watendaji wa kata na wa mitaa watano katika Manispaa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 128 yakiwemo ya wizi wa Sh123 milioni mali ya wananchi wanaomiliki ardhi kata ya Kimara B na Saranga.

Washtakiwa hao na kata zao kwenye mabano ni Missana Ernest aliyekuwa ofisa mtendaji wa kata ya Saranga, Sophia Mwashusa, aliyekuwa ofisa mtendaji wa mtaa wa Stopover, Michungwani na Matangini.

Wengine ni Rahma Tagalile, aliyekuwa ofisa mtendaji wa mtaa wa Upendo kata ya Saranga; Idd Mnyeke, aliyekuwa ofisa mtendaji wa mtaa wa Kimara B na Athuman Mtono, aliyekuwa ofisa mtendaji wa kata ya Kimara B.

Washtakiwa hao, walipandishwa kizimbani leo Alhamisi Oktoba 18, 2018 na kusomewa mashtaka hayo na wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Faraja Sambala, mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ali.

Wakili Sambala amedai washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 128 na kwamba mashtaka 64 kati ya hayo ni ya wizi, wakitumia nafasi zao za utumishi wa umma na mashtaka mengine 64 ni ya ufujaji wa mali.

Sambala amedai kati ya Januari 2012 na Desemba 2013, katika Manispaa ya Kinondoni washtakiwa hao wakiwa watendaji wa kata na mitaa kwa nyakati tofauti waliiba ya Sh 123milioni.

Amedai walitenda makosa hayo, wakati wakijua fedha hizo ni mali ya wenye ardhi waliyopo kata ya Kimara B na Saranga, ambazo zilikuwa mikononi mwao kwa kupitia ajira zao.

Katika mashtaka 64 ambayo ni mbadala ya ufujaji wa mali, Wakili Sambala amedai kati ya tarehe hiyo na sehemu hiyo hiyo washtakiwa kwa pamoja walibadilisha matumizi ya fedha hizo ambazo walikuwa wameaminiwa kupitia nafasi zao na kuzitumia kwa manufaa yao binafsi.

Hata hivyo, washtakiwa walikana mashtaka na Hakimu Ali amewaeleza kuwa dhamana yao iko wazi kwa masharti ya kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh10 milioni na kutotoka nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama.

Hata hivyo, washtakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza mashati ya dhamana.

Hakimu Ali ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 13, 2018 kwa ajili ya kutajwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz