Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watatu wanaswa na meno ya tembo Iringa

Meno Ya Tembo Watatu wanaswa na meno ya tembo Iringa

Fri, 3 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Askari wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (Runapa) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Tanzania limewakamata watu watatu mjini Iringa wakiwa na meno nane mazima ya tembo na vipande sita yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 206.

Watuhumiwa hao ni pamoja na Greyson Lusasi (39) mkazi wa mtaa wa Mwangata mjini Iringa, Elia Halamga (55) mkazi wa Kateshi Manyara na Henry Chengula (38) mkazi wa mtaa wa Isakalilo Iringa mjini.

Akizungumza na wanahabari leo Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Godwell Ole Meing’ataki alisema watuhumiwa hao walinaswa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema zilizoeleza uwepo wa mitandao ya ujangili na biashara ya nyara za serikali.

"Kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi tulitengeneza mtego na kufanikiwa kuwanasa watuhumiwa hao," alisema na kusisitiza kwamba Runapa na Tanapa itaendelea kushirikiana na wananchi wema, Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori na Misitu na Polisi kuwasaka majangiri wa nyara za serikali na kuwafikisha mbele ya vyombo sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Kamishna Msaidizi wa Polisi, Allan Bukumbi alisema watuhumiwa hao walikamatwa Februari 28, mwaka huu majira ya saa 2.30 usiku katika mtaa wa Bombambili Mawelewele mjini Iringa.

Pamoja na meno hayo ya tembo, alisema watuhumiwa hao waliokuwa katika gari aina ya Noah yenye namba za usajili T385 BWG walikutwa pia na jambia moja, msumemo mmoja mifuko ya sulphate mitatu iliyokuwa na meno hayo.

Alisema watuhumiwa hao watakaofikishwa mahakamani hivikaribuni baada ya upelelezi kukamilika walikamatwa wakiwa katika harakati za kutaka kufanya biashara na watu waliokuwa wakiwasiliana nao.

Wakati huo huo jeshi la Polisi limekamata bajaji 140 katika oparesheni yake ya kukamata bajaji zinazovunja sheria za usalama barabarani ikiwemo kuzidisha abiria, kukiuka utaratibu wa leseni ya njia, kutokuwa na leseni za udereva na bima, ubebaji hatarishi wa abiria na mizigo na kuegesha maeneo yasiyoruhusiwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live