Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watatu wanaswa na heroin gramu 400

788bf1e18417da219480ecf9e8337b22 Watatu wanaswa na heroin gramu 400

Thu, 28 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, inawashikilia watuhumiwa watatu kwa kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin.

Watuhumiwa hao ni Mjumbe wa Mtaa wa Kuwaje Kunduchi jijini Dar es Salaam, Kulwa Pazi (49) maarufu Mama Udodi, Emmanuel Maamuzi (21) na Anachati Mchongeza (20).

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (DCEA), James Kaji amesema watuhumiwa hao walikamatwa na gramu 400 za heroin na majani makavu ya bangi kete 30.

“Maofisa wa mamlaka walifanikiwa kukamata kiasi hicho cha dawa zikiwa zimehifadhiwa ndani ya mfuko wa nailoni,” alisema Kaji na kuongeza kuwa watuhumiwa na watafikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

Katika hatua nyingine, Kaji alisema DCEA katika kipindi cha Novemba na Desemba mwaka jana imeshinda kesi tatu ambazo zinawahusisha wafanyabiashara maarufu wa dawa za kulevya nchini.

Kaji alisema kesi hizo zilikuwa zikisikilizwa katika Mahakama ya Makosa ya Uhujumu Uchumi ambako DCEA ilishinda baada ya mahakama hiyo kumtia hatiani Yanga Omari Yanga maarufu 'Rais wa Tanga' na kumhukumu kifungo cha miaka 30 baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha heroin zenye uzito wa gramu 1052.63.

Yanga alikamatwa Agosti, 2018 na wenzake wawili jijini Tanga, wakitaka kusafirisha dawa hizo za kulevya.

Pia mfanyabiashara mwingine aliyetiwa hatiani ni Ayubu Mfaume maarufu 'Kiboko' na mkewe Pili Kiboko ambao wamehukumiwa miaka 20 jela kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 251.25.

Kiboko anadaiwa kuwa kiongozi wa ulanguzi wa dawa ya kulevya aina ya heroin amekuwa akifanya operesheni zake kati ya Afrika Mashariki na China.

“Kiboko ana vijana 68 ambao wameshikiliwa China, ameharibu maisha ya vijana wengi,” alisema Kaji na kueleza kuwa amekuwa na ushirikiano na walanguzi wa mihadarati nchini Brazil, Pakistani na Mataifa ya Ulaya.

Pia raia wawili wa Iran nao wametiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin yenye uzito wa gramu 111.02 katika Bahari ya Hindi na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kutaifishwa kwa jahazi lao.

Chanzo: habarileo.co.tz