Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watatu wafikishwa mahakamani kwa kumiliki radio call ya Serikali

Wafikishwapic Watatu wafikishwa mahakamani kwa kumiliki radio call ya Serikali

Thu, 11 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Watu watatu wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka manane ikiwemo la kumiliki redio ya upepo ya umma.

Washtakiwa hao ni mfanyakazi wa kampuni ya Suma JKT, Michael Funguka, Daniel Shesala ambaye ni mkazi wa Tabata na Steven Lyakurwa.

Wakili wa serikali, Caroline Matemu akisoma hati ya mashtaka leo Novemba 11 mahakamani hapo, amedai kuwa katika shitaka la mwisho linalomkabili Funguka inadaiwa kuwa Oktoba 28 mwaka huu, alikutwa akimiliki redio ya upepo ya umma, huku akijua ni kosa la kisheria.

Ametaja makosa mengine manne ni ya kugushi na matatu ya kutengeneza vifaa vya kugushi.

Matemu amedai katika tarehe isiyojulikana jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Funguka na Shesala wakiwa na nia ya kulaghai walighushi cheti cha udereva kimeandikwa Michael Funguka ikionyesha cheti halali kimetolewa na Chuo cha Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), huku wakijua siyo kweli.

Shtaka la pili, katika tarehe isiyojulikana na maeneo hayo hayo mshtakiwa Funguka na Shesala wakiwa na nia ya kulaghai waligushi cheti cha utambuzi kilichotolewa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) chenye jina la Peter Funguka ikionyesha cheti halali huku wakijua siyo kweli.

Katika shtaka la tatu na la nne tarehe tofauti maeneo hayo washtakiwa hao wakiwa na lengo la kula njama walighushi cheti cha utambuzi kilichotolewa na JKT chenye jina la John Jeremiah.

Matemu amedai shataka la tano hadi la saba, katika tarehe isiyojulikana jijini humo mshtakiwa Funguka na Lyakurwa walitengeneza vifaa vya kugushi ikiwemo muhuri wa mkuu wa chuo cha Makongo, muhuri wa mshauri wa mgambo wa Sumbawanga na muhuri wa moto uliandikwa makao makuu ya JKT Dodoma, huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Baada ya kusomwa mashtaka hayo washtakiwa wote kwa pamoja walikana makosa yanayowakabili.

"Upelelezi bado haujakamilika tunaomba tarehe nyingine," amedai Matemu.

Hakimu Mkazi Mkuu, Ritha Tarimo amesema dhamana ipo wazi hivyo kila mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili wanaoishi jijini Dar es Salaam ambao wawe na barua inayotambulika.

Baada ya kutolewa masharti ya dhamana washtakiwa hao walitimiza masharti hayo na wapo nje kwa dhamana na kesi hiyo imeahirishiwa hadi Novemba 25, 2021 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Chanzo: mwananchidigital