Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watatu waburuzwa kortini kwa utakatishaji bilioni 2/- za NMB

Af6ba1ff7506168ab0c27c3527c4e31b Watatu waburuzwa kortini kwa utakatishaji bilioni 2/- za NMB

Wed, 29 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WATU watatu wamefi kishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka matatu, likiwemo la wizi na utakatishaji wa zaidi ya Sh bilioni mbili mali ya Benki ya NMB.

Washitakiwa hao ni Joseph Nicas (63) Mlinzi na Mkazi wa Kimara, Paston Pangaja (37) Mkazi wa Mbeya na Jacob Mwakyembe (45) dereva ambao wameunganishwa na washitakiwa wengine 20.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni ndugu watano, Manjestus Mselema (44), Bernadetha (45) ambaye ni mama wa nyumbani na Mkazi wa Mbagala, Agnes (29) hotelia, Oswald Mselema (49) na Olaph Mselema (35) wote ni walinzi.

Walinzi wengine ni Beda Mkali (51) ambaye ni CTI Control, Kais Nasibu (35), John Selestine (45), Edes Hyera (43), Engelbert Masare (45), Bernad Victor (39) na Sylidion Odil (42). Pia wapo Tulipo Mwamuzi (40), dereva, Grace Komba (32) Hotelia, Janeth Shilla (59) Wakala wa Kampuni ya Eternal International Ltd, Godwin (52) fundi mwashi na Anold Erio (25), Florah Mwita (25) mfanyabiashara na Tispo Mwasakieni (27) maarufu kama Ronic Kinyozi na mkazi wa Kawe.

Akisoma mashitaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Yusto Ruboroga, Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono alidai washitakiwa hao, Manjestus, Mwakuzi, Godwin, Anold, Agnes, Mwita, Victor na Odil na wenzao wanadaiwa katika tarehe tofauti mwaka huu, 2020, maeneo ya jijini Dar es Salaam walikula njama ya kuongoza genge la uhalifu kufanya kosa la wizi.

Ngukah alidai Juni 8,2020 maeneo ya Mbezi Beach wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote waliiba Sh 2,082,000,000 mali ya Benki ya NMB.

Katika mashitaka ya tatu inadaiwa Juni 8,2020 Mbezi Beach, Kinondoni, Dar es Salaam, washitakiwa wote walijipatia Sh 2,082,000,000 mali ya NMB wakati wakijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa la wizi.

Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.

Upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kukamilisha upelelezi.

Hakimu Ruboroga aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 11, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa wote wamerudishwa rumande kwa sababu mashitaka yanayowakabili hayana dhamana kisheria.

Chanzo: habarileo.co.tz