Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watatu waachiwa huru kesi ya mauaji ya Askari Loliondo

Nyundo Washtakiwa watatu kesi ya mauaji ya askari Loliondo waachiwa huru

Fri, 29 Jul 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Mwanafunzi wa Kidato cha Nne ni miongoni mwa watu watatu kati ya 27 waliofutiwa kesi mauaji ya askari polisi yaliyotokea kufuatia vurugu za kupinga mpango wa Serikali wa kuweka mipaka katika pori tengefu la Loliondo, wilayani Ngorongoro.

Washtakiwa hao wameachiwa huru baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kueleza hana nia ya kuendelea kuwashitaki washitakiwa hao katika shauri hilo.

Jana Julai 28, 2022, Mahakama hiyo ilipanga shauri hilo kwa ajili ya kutoa uamuzi mdogo ambapo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili Upendo Shemkole.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,Fadhil Mbelwa,Wakili Upendo,alieleza mahakama kuwa kuwa DPP hana nia ya kuendelea kuwashitaki washitakiwa hao watatu akiwemo Simeli Parmwati mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ambaye anatakiwa kujiunga na kidato cha tano.

Alisema DPP hana nia ya kuendelea kuwashitaki washitakiwa hao, hivyo wanafutiwa mashtaka chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ( CPA) sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Wengine walioachiwa ni aliyekuwa mshitakiwa namba 22 Fred Ledidi ambaye Julai 14,2022  ilidaiwa mahakamani hapo kuwa ni mwanafunzi anachukua shahada ya uzamivu (PhD), hivyo anapaswa kuwasilisha maandiko yake ya kitaaluma kwa ajili ya kuendelea na masomo hayo.

Mwingine ni Lukerenga Koyee, ambaye ilidaiwa mahakamani hapo kuwa ni mgonjwa ana tatizo la figo.

Baada ya upande wa mashtaka kueleza hayo, Hakimu Mbelwa alikubaliana na ombi hilo na kuwafutia mashtaka na kisha kuwaachia huru.

Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ngorongoro, Ndirango Laizer.

Washitakiwa wengine ni Molongo Paschal, Albert Selembo,Lekayoko Parmwati,Sapati Parmwati, Ingoi Olkedenyi Kanjwel, Sangau Morongeti, Morijoi Parmati,Morongeti Meeki,Kambatai Lulu, Moloimet Yohana,na Joel Clemes Lessonu.

Wengine ni Simon Orosikiria,Damian Rago Laiza, Mathew Eliakimu,Luka Kursas,  Taleng'o Leshoko, Kijoolu Kakeya, Shengena Killel,Kelvin Shaso Nairoti,Wilsom  Kiling,James Taki,Simon Saitoti na Joseph Lukumay.

Hata hivyo uamuzi mdogo haukuweza kutolewa kutokana na Hakimu Mkazi Herieth Mhenga ambaye shauri hilo liko mbele yake kutokuwepo mahakamani hapo.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa mawili ambapo kosa la kwanza ni njama ya mauaji,ambapo kwa tarehe na sehemu isiyofahamika Ngorongoro,walipanga njama ya kuua maafisa wa serikali na maafisa polisi watakaoshiriki zoezi la kuweka mipaka pori tengefu la Loliondo.

Kosa la pili ni mauaji ambapo wanadaiwa Juni 10,2022 eneo la Ololosokwan,wilayani Ngorongoro kwa nia ovu walisababisha kifo G 4200 Koplo Garlus Mwita.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 5, 2022.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz