Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watatu mbaroni kwa kupeleka nje vinyonga 74, nyoka 6

6394ecf670909edde311841904743480 Watatu mbaroni kwa kupeleka nje vinyonga 74, nyoka 6

Fri, 12 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATANZANIA watatu wamekamatwa wakituhumiwa kushirikiana na raia wa Jamhuri wa Czech kusafirisha nje ya nchi vinyonga 74 na nyoka 6.

Waziri wa Maliasili na Utali, Dk Damas Ndumbaro jana aliwaeleza waandishi wa habari mjini Iringa kuwa, maofisa wa forodha wa Austria walikamata vinyonga na nyoka hao wakiwa kwenye begi ambalo ndani yake waliwekwa kwenye soksi na kuingizwa kwenye vifungashio vya plastiki.

Dk Ndumbaro alisema, watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani kesho na kwamba, watakabiliwa na mashitaka ya kusafirisha nje wanyamapori bila kibali, uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.

Alisema, vinyonga na nyoka hao walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Vienna nchini Austria na inadaiwa walitoka katika milima ya Usambara, Tanzania.

Dk Damas Ndumbaro alisema baada ya kupata taarifa kupitia mitandao ya kijamii, wizara kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na kwa kutumia kikosikazi dhidi ujangili iliunda kikosi maalumu kuchunguza tukio hilo.

Alisema kupitia taarifa za kiintelijensia kikosi maalumu kilipata jina la mtuhumiwa aliyesafirisha vinyonga hao ambaye raia wa Jamhuri ya Czech.

Dk Ndumbaro alisema, uchunguzi unaendelea ili kubaini namna vinyonga na nyoka walivyopitishwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) bila kugundulika.

Alisema watuhumiwa watakaobainika kuhusika na uhalifu huo wataunganishwa na wenzao ambao tayari wamekamatwa. Dk Ndumbaro alisema serikali itashirikiana na nchi ya Austria katika uchunguzi unaoendelea ikiwa ni pamoja na kuwarudisha Tanzania vinyonga na nyoka hao.

Alisema, serikali pia itawasiliana na Jamhuri ya Czech ili watuhumiwa ambao ni raia wake wachukuliwe hatua.

Dk Ndumbaro alisema serikali inakusudia kuifuta kabisa biashara ya wanyamapori hai ambayo ilizuiwa tangu Mei, 2016.

Chanzo: www.habarileo.co.tz