Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watatu mbaroni kwa kufanya kazi nchini bila vibali Arusha

Tue, 13 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Raia watatu wa kigeni wamekamatwa kwa tuhuma za kufanya kazi nchini katika kampuni ya Hanspaul Industries Limited Tanzania bila vibali kutoka mamlaka husika wakati wa operesheni ya serikali ya kusimamia utekelezaji wa sheria za ajira na usalama eneo la kazi.

Kamishna wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Gabriel Malata aliongoza Operesheni hiyo ambayo ilibaini kasoro mbalimbali zikiwemo wafanyakazi hao wa kigeni waliokua wakitumia vibali vya Visa za Biashara(BV) badala ya vibali vya kazi kuwa ni kosa kisheria.

Wafanyakazi hao ni Ralph Leopold Hruschka raia wa Ujerumani, Shiva Kumar Vemula raia wa India na Vinoth Krishanth Sathasivam raia wa Sri Lanka pamoja na Mkurugenzi wa kampuni hiyo,Dharam Singh Hanspaul walifikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi kwaajili ya kuandika maelezo.

"Kitendo cha raia wa kigeni kufanya kazi nchini bila kufuata taratibu za kisheria kinaweza kuhatarisha usalama wa nchi pia kinainyima serikali mapato kwani Visa ya biashara ni dola 200 kwa mwezi sawa na Sh 450,000 wakati kibali cha kazi ni dola 700 sawa na Sh 1,575,000,"alisema Malata

Akiwa katika kampuni ya Lodhia Steel Industries Ltd alitoa siku 14 kuhakikisha wafanyakazi wote wanakua na mikataba ya ajira, wanafaa mavazi rasmi ya kazi kulingana na mazingira ya kazi zao pamoja na mwajiri kuhakikisha wafanyakazi wanajiunga na mfuko wa hifadhi ya Jamii wa NSSF na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi(WCF).

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Sailesh Pandit alisema wana jumla ya wafanyakazi 478 kati yao raia wa kigeni wapo 13 ambao wote wana vibali halali vya kufanya kazi nchini na kuwa wafanyakazi sita ambao hawana mikataba ndani ya muda waliopewa itakua imeandaliwa.

Katika hoteli ya Ngurdoto Mountain Lodge iliyopo wilayani Arumeru pamoja na mambo mengine baadhi ya wafanyakazi mikataba yao ya ajira haikuwa imehuishwa, michango yao kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii haikuwa imewekwa kila mwezi na hawana chama cha wafanyakazi.

Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Laissser Ole Mattasia alisema changamoto zilizojitokeza zitafanyiwa kazi na kutolewa taarifa katika kipindi cha mwezi mmoja kwani kampuni yake ina heshimu sheria za nchi na itahakikisha maagizo yote yanatekelezwa.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz