Dar es Salaam. Watu watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumanne Mei 21, 2019 wakikabiliwa na mashtaka mawili, likiwemo la kukutwa na vipande vya meno ya tembo yenye thamani ya Sh69milioni.
Wakili wa Serikali, Candid Nasua amewataja washtakiwa hao kuwa ni Godlisten Mtume (31), Frank Lucas(24) na Mhando Shomary (37).
Akiwasomea hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde, Nasua amedai washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 40/2019.
Amedai katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Mei 7, 2019 Mbezi Luis jijini Dar es Salaam walikutwa na vipande vinne vya meno ya tembo vyenye thamani ya dola 30,000 za Marekani sawa na Sh69milioni mali ya Serikali ya Tanzania.
Nasua amedai washtakiwa hao walikutwa na vipande hivyo bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori nchini.
Katika shtaka la pili, siku na eneo hilo, washtakiwa walitakatisha Sh69milioni, fedha zilizotokana na malipo ya uwindaji.
Pia Soma
- Waziri wa zamani Tanzania ajutia uamuzi wake, adai uliwaumiza wavuvi
- Mahakama Moshi yatupa pingamizi la wakili kesi ya bilionea Olomi
- Mbunge CUF adai akimsalimu Waziri Mpina hamjibu
Nasua amedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na Hakimu Kasonde kuahirisha shauri hiyo hadi Juni 4, 2019.