Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watatu kortini kesi ya vinyonga wa mil 9/-

Df229e5450d8ee50c7dbe7a9725d8023.jpeg Watatu kortini kesi ya vinyonga wa mil 9/-

Wed, 17 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATU watatu wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kuongoza genge la uhalifu na kujihusisha na biashara ya nyara za serikali bila kibali cha Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori.

Washitakiwa hao Erick Ayo, Alli Ringo na Azizi Ndago, walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mawili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaid.

Katika shitaka la kwanza, Wakili wa Serikali, Kija Luzungana, alidai washitakiwa hao kati ya Desemba 22 mwaka jana na Februari 21, mwaka huu katika maeneo tofauti ndani ya mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Tanga na Pwani kwa pamoja na kwa makusudi, walishirikiana kuongoza genge la uhalifu na kusafirisha vinyonga wenye thamani ya Sh 8,546,889 mali ya Serikali ya Tanzania.

Luzungana alidai mahakamani kuwa, katika shitaka la pili washitakiwa wote kwa pamoja na kwa makusudi wakiwa na nia ya kujipatia faida, walijihusisha na biashara ya nyara za serikali kwa kusafirisha vinyonga 74 wenye thamani Sh 8,546,889.

Ilidaiwa mahakamani kuwa, walitenda kosa hilo kati ya Desemba 22 mwaka jana na Februari 21, mwaka huu katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Tanga, na Pwani.

Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 29, 2021 itakapotajwa.

Washitakiwa walipelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kupeleka wadhamini wawili wenye vitambulisho waliotakiwa kusaini bondi ya Sh milioni 2 kila mmoja na mmoja kati yao, awasilishe hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz