Jeshi la Polisi mkoani Dodoma, Tanzania linawashikilia watu watano kwa mauaji ya watu watano wa familia moja yaliyogundulika Januari 15, 2022 katika kijiji cha kijiji cha Zinka wilayani Bahi mkoani Dodoma.
Waliogundulika kuuawa Januari 15, 2022 katika kijiji hicho, wanandoa Hosea Kapande na Paulina Kalonga pamoja na watoto wao Agnes na Isaka pamoja na mjukuu wao Heltone.
Watu hao walizikwa Jumapili Januari 16, katika makaburi ya familia yaliyopo karibu na nyumba hiyo kulikofanyika mauaji.
Kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma Onesmo Lyanga amesema kuwa wanaowahoji ni pamoja na ndugu wa familia hiyo.
“Tunafanya mahojiano na watu kadhaa. Tunafanya mahojiano na watu watano,”amesema kamanda Lyanga.
Alipoulizwa kama wanaohojiwa wote ni ndugu, Lyanga alijibu “hapana ni mchanganyiko.”
Akizungumza katika eneo la tukio Jumamosi jioni, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka aliwataka wakazi wa kijiji hicho pamoja na ndugu kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili waliofanya kitendo hicho wajulikane na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Hili jambo litakuwa limefanywa kwa ushirikiano na watu wa hapa, hawezi kuja mtu kutoka huko akaja kwenye nyumba ya mtu akauwa watu watano asiwe na mwenyeji hapa,” amesema.
Aliagiza vyombo vyote vya ulinzi na usalama na uchunguzi vyote mkoa kuhamia katika kijiji hicho kufanya uchunguzi wa tukio hilo na waone namna ya kushirikiana na wenzao kama italazimika kufanya hivyo.
“Ni lazima hawa watu wapatikane, ni lazima. Labda muwe wanafiki, naomba wananchi watoe ushirikiano. Hii ni damu ya watu watajisema tu,” amesema.