Morogoro. Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linawashikilia waganga watano wa kienyeji kwa tuhuma za kupiga ramli chonganishi.
Mbali na kuwakamata, polisi wamezuia jaribio la ndugu kuwahamisha wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya rufaa mkoani Morogoro kuwapeleka kwa waganga hao.
Akizungumza leo Alhamisi Julai 11, 2019 kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro, Willbrod Mutafungwa amewataja kuwa ni Idd Mpuye maarufu Dk Makata, Athumani Ramadhani maarufu Dk Simba, Chande Rajabu (mtoto wa Simba), Mussa Kombo (Mchinja) na Seif Lindoi maarufu Dk Kipara, wote wakazi wa Dar es Salaam.
Amesema waganga hao walikuwa wakipiga ramli chonganishi na kutoa majini kwenye nyumba za wakazi wa kata ya Chamwino kwa Sh 5000 kila nyumba huku wakidai kuna mapembe yaliyowekwa na majirani au ndugu.
“Tulipopata taarifa tulifika katika maeneo hayo na kukuta makundi ya watu yakiwafuatilia waganga hao ili waone mapembe yanayotolewa kwenye nyumba za watu kitendo ambacho kinahatarisha amani baina ya majirani na ndugu,” amesema kamanda huyo.
Amesema waganga hao walipopekuliwa walikutwa na matunguli, vioo, mtambo unaoonesha sura za wachawi, dawa mbalimbali pamoja na Sh231,000, noti mbili za zamani na fedha ya Zambia Kwacha 1,000.
Pia Soma
- Benki ya UBA Tanzania yasaidia vitabu shule za Sekondari wilayani Kigamboni
- Muungano wa Tigo na Zantel utakuza uchumi nchini
- TEF waitaka Serikali ya Tanzania kutoa maelezo kuhusu Azory Gwanda
- Mwamunyage amshukia mkandarasi Kisarawe
Hata hivyo, walikiri kutokuwa na vibali vya kufanya kazi hiyo huku wakibaisha kuwa wenyeviti wa Serikali za mitaa wanajua ujio wao.