Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watano kortini wakidaiwa kukwepa kodi ya Sh139 milioni

70660 Pic+kortini

Sat, 10 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wafanyabiashara watano wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kukwepa kodi.

Washtakiwa hao wanadaiwa kukwepa kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kiasi cha Sh139 milioni baada ya kuingiza nchini magari 26 kutoka Japani.

Washtakiwa hao ni Edwin Bisama (35); Stephen Murashani; Idd Abdallah; Emmanuel Allen na Elizabeth Eben.

Wakili wa Serikali, Glori Mwenda amedai leo Ijumaa Agosti 9, 2019 kuwa  washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 58/2019.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Salum Ally  wakili Mwenda amedai katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote wanadaiwa kula njama za kukwepa kodi.

Katika shtaka la kukwepa kodi, Mwenda amedai tarehe tofauti kati ya Juni 2018 na Januari 2019 jijini Dar es Salaam washtakiwa kwa pamoja walishindwa kulipa kodi ya magari 26 waliyoyaingiza nchini ambayo ni Sh139.5 milioni.

Pia Soma

Katika shtaka la tatu ambalo ni kuisababishia hasara TRA, washtakiwa kwa pamoja siku na eneo hilo, kwa hiari yao walishindwa kulipa kodi hiyo ya magari na kuisababishia TRA  hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Washtakiwa hao pia wanadaiwa kutakatisha fedha haramu kiasi cha  Sh139.5 milioni.

Baada ya kusomewa mashtaka yao, hawakutakiwa kusema chochote mahakamani hapo kutokana na baadhi ya mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana kisheria.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi bado haujakamilika kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Ally ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 23, 2019 kesi hiyo itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Imeandikwa na Hadija Jumanne, Faraji  Issah na Rebecca John

Chanzo: mwananchi.co.tz