Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watano kizimbani wakidaiwa kujipatia Sh26 milioni kwa kuingilia miamala ya fedha

69580 Pic+miamala

Sat, 3 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hamisi Singa (30), raia wa Burundi na Watanzania wanne wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka saba, likiwemo la kuingilia mfumo wa taarifa za miamala ya fedha za mawakala  na kutakatisha fedha Sh26 milioni.

Mbali na Singa  ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya mawasiliano ya Tigo,  washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 72/2019  ni Jailos Joseph, Singa Mnunga, Japhet Mkumbo na Omari Omari.

Wamefikishwa mahakamani hapo leo Ijumaa Agosti 2, 2019 na kusomewa mashtaka yao na wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salum Ally.

Akisoma mashitaka hayo, Simon amedai kati ya Januari na Julai, 2019 mkoani Arusha, Manyara na maeneo mengine nchini, washitakiwa wote walikula njama ya kutenda kosa la kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.

Katika shtaka la pili, siku na maeneo hayo, washtakiwa hao kwa ulaghai walijipatia Sh26 milioni kupitia miamala ya wateja wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom na Airtel.

Simon aliendelea kudai katika shtaka la tatu, washtakiwa kwa pamoja walisambaza taarifa za uongo kupitia ujumbe wa mfupi wa maandishi usomekao 'Tuma Pesa kwa namba Hii'  kwa lengo la kuhadaa umma wa Watanzania.

Pia Soma

Katika shtaka la nne, wote wanadaiwa kuanzisha na kusambaza ujumbe mfupi wa maneno ambao haujaombwa kupitia laini zao za simu za mkononi ambazo wamezisajili kwa majina ya watu wengine.

Simon amedai shtaka la tano, washtakiwa  hao  wanadaiwa kusambaza ujumbe huo kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu wakati wakijua ni kinyume cha sheria.

Katika shtaka la sita, ambalo linamkabili Hamisi anadaiwa kuwa  akiwa mwajiriwa wa kampuni ya Tigo , aliingilia taarifa mbalimbali za miamala ya fedha za mawakala wa Tigo kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Simon aliendelea kudai kuwa katika shtaka la saba, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutakatisha fedha haramu kiasi cha Sh26 milioni wakati wakijua fedha hizo zilitokana na kosa la jinai ambalo ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Hata hivyo, washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana kisheria.

Hakimu Ally ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 15, 2019  itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Chanzo: mwananchi.co.tz