Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Watajeni wanaume teleza’

59736 Pic+teleza

Sun, 26 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigoma. Mkuu wa Mkoa Kigoma, Emmanuel Maganga amewataka wazee wanaoishi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji kushirikiana na jamii nzima kuwafichua kwa kuwataja vijana wanaojiita wanaume teleza kwa vile wanaishi katika nyumba zao na wanawafahamu.

Maganga alitoa kauli hiyo juzi wakati wa futari aliyoandaa nyumbani kwake kwa ajili ya wakazi wa manispaa hiyo.

Wanaume teleza ni jina linalotumika kuwatambulisha vijana wanaofanya vitendo vya uhalifu nyakati za usiku ambao huvunja milango, kuiba na wakati mwingine kubaka wanawake.

Alisema jamii ikitoa ushirikiano, vijana hao watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na wakipatikana na hatia watafungwa gerezani.

Aliwataka kuacha woga kwa kuficha taarifa juu ya unyama unaofanywa na vijana hao na kulifanya jambo hilo kuchukuliwa kwa ukubwa tofauti na hali ilivyo.

“Toeni taarifa Polisi ili hao vijana wakamatwe, lakini kama mnaogopa kuwaambia Polisi njooni kwangu na mnitajie majina yao na nitahakikisha wanakamatwa na kufikishwa mahakamani,” alisema Maganga.

Pia Soma

Diwani wa Mwanga Kusini, Mussa Maulidi alisema ikiwa jamii itakuwa tayari kutoa taarifa Polisi, tatizo hilo litakwisha na watu kuishi kwa amani.

“Hawa wanaume teleza dhamira yao kubwa huwa ni kubaka wanawake kwa sababu nyumba wanazovamia ni zile wanazoishi kina mama tena mabinti vijana ambao hawana waume, wanapoingia ndani hulazimisha kuwabaka na wakikubali kubakwa hakuna kelele,” alisema Maulidi.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Ottieno alisema baadhi ya watu katika jamii ni kichocheo cha vitendo hivyo vya uhalifu kwa vile licha ya kuvamiwa na kuumizwa wamekuwa wakimaliza kesi nje ya vyombo vya sheria.

Alisema tangu mwaka 2016 hadi Mei 2019 kuna kesi 13 zinazohusu wanaume teleza na zote ni za kujeruhi na shambulio la kudhuru mwili, “hakuna kesi yoyote inayohusu ubakaji iliyoripotiwa Polisi, kesi zote za hao teleza ni kuvunja, kujeruhi na kudhuru mwili.”

Mkazi wa Mwanga, Issa Jumapili alisema wanaume teleza ni vijana wabakaji na lazima jamii ishirikiane na vyombo vya sheria kuwadhibiti.

Pia, Amisa Feruzi wa Kilimahewa alisema wanaume teleza wanafahamika lakini baadhi ya watu wanaogopa kuwataja kwa kuhofia usalama wao.

Chanzo: mwananchi.co.tz