Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Washtakiwa watumishi wa Mahakama waongezewa muda wa ‘plea bargaining’

Hukumu Pc Data Washtakiwa watumishi wa Mahakama waongezewa muda wa ‘plea bargaining’

Thu, 19 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mtwara imewaongezea muda wa siku 14 watumishi watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara wanaokabiliwa na kasi tatu tofauti za uhujumu uchumi kuendelea kufanya majadiliano ya makubaliano, (Plea Bargaining) na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), katika kesi moja.

Washitakiwa hao ambao ni wahasibu wawili, Beda Nyasira (47), Theodosia Mtelani (37) na mtunza kumbukumbu, Mahafudhi Chinenda (42).

Mahakama hiyo imewaongezea muda huo washtakiwa hao baada kuombwa na wakili wao, anayewatetea, Alex Msalenge, kufuatia muda waliopewa awali katika kesi ya uhujumu uchumi namba 4 ya mwaka 2023 kuisha bila kufikia muafaka.

Kesi hiyo pamoja na nyingine mbili ambazo zote zinasikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi,

Charles Mnzava, zilitajwa mahakamani hapo jana/uzi Oktoba 18, 2023 ndipo wakili wa washtakiwa hao, Msalenge akaiomba mahakama hiyo kuwapa muda wa nyongeza kwa ajili ya kuendelea na majadiliano hayo, katika kesi hiyo.

Hakimu Mnzava alikubaliana na ombi hilo, akawaongezea siku 14 hadi Novemba Mosi, 2023, tarehe ambayo kesi hiyo pamoja na nyingine mbili zitatajwa tena mahakamani hapo.

Awali katika kesi hiyo namba 4 mahakama hiyo iliwapa siku 30, kama kanuni za majadiliano hayo zinavyoelekeza; kuanzia Septemba 11, 2023 hadi Oktoba 11, 2023 muda wao ulipoisha.

Katika kesi hiyo washatakiwa hao wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 19 likiwemo la kutakatisha fedha haramu zaidi ya Sh56 milioni zilizokuwa kwenye akaunti maalum ya mahakama kuu Kanda ya Mtwara iliyopo Benki Kuu ya Tanzania, (BOT) ambazo ni za wanufaika wa mirathi.

Pia washtakiwa hao wako katika majadiliano na DPP katika kesi nyingine namba 5 ya mwaka 2023, ambayo muda wa awal waliopewa na mahakama wa siku 30 kwa mujibu wa kanini hizo utaisha Oktoba 25, 2023.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wote kwa pamoja wanakabiliwa na makosa mbalimbali likiwemo la ubadhirifu wa fedha kiasi Sh20.7 milioni.

Kuhusiana na kesi nyingine ya tatu, kesi namba 6 ya mwaka 2023, wakili Alex aliieleza mahakama hiyo jana kuwa washitakiwa hao wana nia ya kufanya majadiliano na DPP, ambayo pia mahakama imewapa siku 30.

Katika kesi hiyo washtakiwa wote wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 14 ambayo ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka, kuitia mamlaka hasara, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi cha Sh56.2 milioni kinyume cha sheria.

Wanadaiwa kuwa walitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Juni 2020 na Mei 2022.

Washitakiwa hao kwa pamoja walifikishwa mahakamani hapo kwa nyakati tofauti na kusomewa mashtaka hayo katika kesi hzio tatu tofauti za uhujumu uchumi zinazohusisha zaidi ya Sh132 milioni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live