Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Washtakiwa uhujumu uchumi waijaza Serikali Sh40 bilioni

80119 Uchumi+pic

Tue, 15 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Washitakiwa 24 wa kesi za uhujumu uchumi wameomba msamaha na kukubali kurejesha fedha wanazodaiwa kuzihujumu.

Kupitia washitakiwa hao wanaotokana na kesi 10 za uhujumu uchumi, Serikali inatarajia kuvuna Sh39.744 bilioni zikiwa ni fidia ambayo washtakiwa wamekubali kuilipa Serikali.

Hatua hiyo ya kukiri makosa na kuwa tayari kurejesha fedha imekuja baada ya siku 14 za msamaha alizotoa Rais John Magufuli kwa washtakiwa hao kuomba msamaha na kurejesha pesa wanazodaiwa.

Rais Magufuli alitoa msamaha huo Septemba 22, mwaka huu, alipomshauri Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Biswalo Mganga kuangalia uwezekano wa kuwasikiliza washtakiwa wa makosa ya uhujumu uchumi ambao wako tayari kuomba radhi na kurejesha pesa wanazodaiwa.

Oktoba Mosi DPP, alitoa taarifa kwa Rais kuwa hadi siku hiyo washtakiwa 467 waliandika barua kuomba msamaha na wako tayari kurejesha pesa wanazodaiwa, zinazofikia Sh107 bilioni.

DPP pia alisema kuna washtakiwa wengine wameonyesha nia ya kuandika barua lakini wamechelewa kutokana na sababu mbalimbali hivyo alimuomba Rais amuongezee siku tatu zaidi na Rais Magufuli akaridhia kwa kumuongezea siku saba badala ya tatu.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Msamaha wa Rais Magufuli ulikuja wakati tayari Bunge la Tanzania lilishafanya marekebisho katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kwa kutoa fursa ya majadiliano baina ya DPP na washtakiwa katika baadhi ya makosa ya jinai yakiwemo ya uhujumu uchumu.

Majadiliano hayo yanalenga kumwezesha mshtakiwa kukiri makosa na kutoa taarifa zitakazowezesha kuzuia makosa mengine au ili kuharakisha kesi ili aweze kushtakiwa kwa kosa lenye adhabu ndogo kati ya mengi au kuondolewa baadhi ya mashtaka au yote.

Hata hivyo mwisho wa majadiliano hayo lazima makubaliano ya pande zote yawasilishwe mahakamani na kusajiliwa baada ya mahakama kujiridhisha kuwa ni ya hiyari kabla ya kutoa uamuzi.

Pia baada ya makubaliano hayoa, mahakimu na majaji wanaosikiliza kesi hizo wanawaelezawashtakiwa haki walizozipoteza kwa kufikia makubaliano hayo kwa mtindo wa kuwauliza maswali.

Haki hizo ni pamoja na haki ya kusikilizwa, yaani kujitetea, haki ya kukata rufaa kupinga hukumu ya mahakama baada ya kuwatia hatiani. Maana yake ni kuwa hawawezi kukata rufaa kupinga kutiwa hatiani bali wanaweza kuwa na haki ya kukata rufaa kupinga tu adhabu hasa faini.

Washtakiwa ambao tayari wamepokea msamaha kwa kukiri mahakamani na kurejea uraiani na pesa wanazopaswa kurejesha zikiwa kwenye mabano ni...

Dk Tenga na wenzake (Sh8.54 bilioni)

Ni viongozi wa kampuni ya mawasiliano ya Six Telecoms Ltd, akiwemo wakili Dk Ringo Tenga, ambaye ni mkurugenzi na mwanasheria wa kampuni hiyo na wenzake, wanne.

Walikuwa wakikabiliwa na mashtaka sita, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, likiwemo la kutakatisha fedha na kuisababishia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) hasara ya Dola 3.7 milioni (zaidi ya Sh8.5 bilioni ).

Wengine ni Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte Peter Noni, Noel Chacha na Frank Mwalongo.

Oktoba 7, Mahakama ya Kisutu iliwaamuru kulipa fidia ya kiasi hicho cha fedha na tayari wamelipa malipo ya awali Dola 150,000 na mahakama iliwaamuru kulipa fedha iliyobaki Dola 3.5 milioni ndani ya miezi sita lakini pia nyumba iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam iliyokuwa ikimilikiwa na washtakiwa ilitaifishwa na kuwa ya serikali.

Wambura (Sh100 milioni)

Alikuwa Makamu wa Rais wa Shirikiksho la Soka Tanzania (TFF), alikuwa akikabiliwa na mashtaka 17 ya kughushi, kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo; kujipatia fedha kwa udanganyifu Sh100 milioni na kutakatisha fedha kiasi hicho.

Mahakama ya Kisutu ilimwamuru kuilipa Serikali Sh100 milioni kwa awamu tano, Sh20 milioni kila awamu kuanzia Oktoba 7, 2019 hadi Septemba 30, 2020, na ilimwachia huru kwa sharti la kutokutenda kosa lolote ndani ya miezi 12.

Mkurugenzi Bank M (Sh6 bilioni)

Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Bank M, Sanjeev Purushothaman, raia wa India, alikuwa akikabiliwa na mashtaka 29 yakiwamo kutakatisha fedha, kughushi na kujipatia fedha kwa udanganyifu zaidi ya Sh6 bilioni.

Oktoba 8, Mahakama ya Kisutu ilimuamuru kuilipa Serikali fidia zaidi Sh6 bilioni na kulipa faini ya Sh2 milioni. Tayari amelipa pamoja na Sh690 milioni, na kiasi kilichobaki ametakiwa kulipa kwa awamu kwa miezi 24.

Meneja TWB (Sh153 milioni)

Meneja huyo wa zamani wa Benki ya Wanawake (TWB), Priscus Shirima, alikuwa akikabiliwa na mashtaka matatu ya wizi kufanya miamala ya pesa ya uwongo, utakatishaji fedha Sh120 milioni.

Oktoba 8, Mahakama ya Kisutu iliamuru ailipe Serikali Sh153 milioni na faini Sh1 milioni. Ameshalipa Sh10 milioni na kiasi kilichobaki atalipa ndani ya miezi mitatu.

Mshirika na mhasibu wa Takukuru (Sh100 milioni)

Yasin Katera, mshtakiwa wa nne katika kesi ya aliyekuwa mhasibu wa Takukuru, Godfrey Gugai.

Katera kabla ya kukiri na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtaka 43 likiwemo la kumiliki mali zisizo na maelezo zenye thamani ya zaidi ya Sh3.6 bilioni.

Katera alikiri makosa yake na Mahakama ya Kisutu ikamtaka kulipa faini ya Sh100 milioni au kwenda jela miaka mitatu. Pia mahakama ilitaifisha nyumba zake mbili za Nyegezi Mwanza na kuwa mali ya Serikali.

Katera ameondolewa katika kesi hiyo lakini wenzake Gugai, George Makaranga na Leonard Alloys wanaendelea kukabiliana na mashtaka yao wakisubiri hukumu baada ya kukamilisha usikilizwaji.

Mkurugenzi Aste Insurance Brokers na Vigogo wa Nida (Sh293.4 milioni)

Ni Astery Ndege, mkurugenzi kampuni ya Aste Insurance Brokers, aliyekuwa mshtakiwa wa tatu katika kesi ya Uhujumu Uchumi iliyokuwa ikimkabili na vigogo wa Mamlaka ya Vitambulisho (Nida), akiwemo aliyekuwa mkurugenzi wa Nida, Dickson Maimu.

Oktoba 8, mwaka huu, Mahakama ya Kisutu imemuamuru kuilipa Serikali Sh293.4 milioni na kumtaka kulipa kwanza Sh50 milioni kama malipo ya awali, ikiwa ni sehemu ya hasara ya Sh1.175 bilioni, iliyosababishwa na washtakiwa wote.

Washtakiwa waliobaki katika kesi hiyo ni Maimu, Aveln Momburi (aliyekuwa meneja biashara Nida), George Ntalima Sabina Raymond na Xavery Kayombo. Kesi hiyo imepangwa kutajwa Oktoba 15 mwaka huu kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa.

Mashtaka yanayowakabili ni kuisabishia Serikali hasara Sh1.175 bilioni, utakatishaji fedha, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo ili kumdanganya mwajiri, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Askari wa wizi wa mafuta ya ndege (Sh4.647 milioni)

Washtakiwa ni askari polisi watano na mwanajeshi mmoja wa Jeshi la Ulinzi (JWTZ). Askari ni Koplo Shwahiba, PC Elidaima Paranjo, PC Simon, PC Dickson, PC Hamza na Ally Chibwana ambaye ni mwanajeshi. Walikuwa wakikabiliwa na mashtaka matatu ya kupanga uhalifu, wizi wa lita 2,180 za mafuta ya ndege yenye thamani ya Sh4.6milioni na utakatishaji fedha.

Oktoba 5, walikiri mashtaka yao na mahakama iliwaamuru kuilipa Serikali fidia zaidi ya Sh4.647 milioni na kutaifisha madumu 109 yaliyotumika kuweka mafuta hayo.

Kusafirisha kobe (Sh40 milioni)

Kesi hii inawakabili wakazi watano wa Zanzibar, David Mungi, Mustafa Bakar, Mohammed Seleman, Salum Wakili na Shaban Haji, ambao ni wafanyabiashara na wavuvi. Wanadaiwa kupokea na kusafirisha kobe 201 aina ya India wa thamani ya Sh30 milioni, ambao ni nyara za Serikali bila kibali, wakidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Novemba 1 na 16 katika maeneo tofauti Dar es Salaam na Zanzibar.

Oktoba 8, Mahakama ya Kisutu iliwaamuru kulipa fidia Sh40 milioni ambazo walifanikiwa kulipa.

Mvietnam, Bui (Sh22 milioni)

Machi 3, 2018, Bui alidaiwa kukutwa na nyara za Serikali ambazo ni kucha 98, meno 21, mifupa 12 vyote vya Simba vya thamani ya Dola 4,900 (zaidi ya Sh11 milioni), katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), bila kibali.

Mahakama ilimwamuru kulipa faini ya Sh22.1 milioni au kwenda jela miaka 15 ambako kupitia wakili wake aliahidi kulipa faini.

Kuiibia Serikali Sh7 milioni kwa dakika (Sh24.6 bilioni)

Mfanyabiashara Mohamed Mustafa Yusufali na wenzake wawili, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama Mahakama ya Ufisadi.

Mbali na Yusufali aliyewahi kutajwa na Rais Magufuli kuwa anaiibia Serikali Sh7 milioni kwa dakika, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Farm Plant Ltd, wengine ni Arifal Paliwalla, aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni hiyo na Sameer Khan, aliyekuwa meneja wa benki ya I&M, tawi la Kariakoo.

Wote walikuwa wakikabiliwa na mashtaka 544 yakiwemo ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uwongo na kutoa taarifa za uwongo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kukwepa kodi, utakatishaji fedha na kuisababishia TRA hasara ya zaidi ya Sh24.3 bilioni.

Oktoba 11, DPP aliwapunguzia mashtaka na kubakia na mashtaka matatu ya udanganyifu uliosababisha kukwepa kodi na ukwepaji kodi yote yakimhusu Yusufali na shtaka la tatu la kuisababishia TRA hasara ya Sh24.3bilioni kwa washtakiwa wote.

Baada ya hapo walisomewa upya mashtaka hayo ambayo wote waliyakiri kisha mahakama ikawatia hatiani na kuwahukumu faini na kulipa fidia kwa mujibu wa makubaliano waliyofikia na DPP.

Mahakama hiyo ilimwamuru Yusufali kuilipa TRA fidia ya Sh24.3 bilioni kodi aliyokwepa na ikaamuru mali zake yaani nyumba zake nne mbili zilizoko Masaki Dar es Salaam na mbili zilizoko Bagamoyo zitaifishwe na kuwa mali ya Serikali. Tayari ameshalipa Sh1 bilioni na kiasi kilichobaki atapaswa kukilipa ndani ya miezi 24 yaani Sh970.9 milioni kila mwezi.

Mshtakiwa wa pili Paliwalla alitakiwa kulipa fidia ya Sh10 milioni na ameshalipa Sh1 milioni na Sh9 milioni zilizobakia atazilipa ndani ya miezi 12 kwa kiasi cha Sh750,000 kila mwezi.

Mshtakiwa wa tatu. Khan ameamuriwa kulipa fidia ya Sh300 milioni, ameshalipa Sh200 milioni hivyo Sh100 milioni zilizobaki atazilipa ndani ya miezi 10 yaani Sh10 milioni kila mwezi.

Paliwalla na Khan tayari wamesharudi uraiani na kumwacha Yusufali kwa kuwa bado anakabiliwa na kesi nyingine ya kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh2.9 bilioni yeye na wenzake wengine wawili, ambayo nayo ameshaandika barua kwa DPP kukiri mashtaka.

Chanzo: mwananchi.co.tz