Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Washtakiwa meno ya tembo upelelezi bado

44838 PIC+MENO Washtakiwa meno ya tembo upelelezi bado

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watu watano wakiwemo wanawake wawili katika kesi ya kukutwa na vipande 18 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh171. 8 milioni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaendelea kusota katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matano katika kesi ya uhujumu namba 94/2018 likiwemo la utakatishaji wa fedha.

Washtakiwa hao ni Salehe Majaliwa (31) mfanyabiashara na mkazi wa Kigamboni na Mwanaisha Ndwangila (36), mkazi wa Tunduru, Sauda Athuman (36) maarufu kama Kipeleka na mkazi wa Mbagala; Hamisi Ulega (27) mkazi wa Lindi na dereva, Abdallah Mohamed (38) maarufu kama Bambo, mkazi wa Kilwa Masoko mkoani Lindi.

Wakili wa Serikali, Elizabeth Mkunde ameieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi, Mwanjah Hamza kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika hivyo aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Hamza ameahirisha shauri hilo hadi Machi 18, 2019 itakapotajwa tena.

Inadaiwa katika shtaka la kwanza mshtakiwa wa kwanza hadi wa nne katika tarehe tofauti, kati ya Novemba Mosi na Novemba 21, 2018, katika mkoa wa Dar es Salaam na Lindi, kwa pamoja walishiriki kuuza nyara za Serikali, ambazo ni vipande 18 vya meno ya tembo, vyenye thamani ya Dola 75,000 sawa na Sh171, 796, 500, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Katika shtaka la pili, ambalo pia ni kuongoza mtandao wa uhalifu, linalowakabili Mwanaisha na Mohamed, inadaiwa siku hiyo na eneo hilo, washtakiwa hao walitoa fedha Sh171, 796, 500, ambazo zilisaidia kununua vipande 18 vya meno ya tembo.

 

Iliendelea kudaiwa, katika shtaka la tatu, ambalo ni la kukutwa na meno ya tembo linalomkabili Majaliwa peke yake, inadaiwa Novemba 21, 2018 katika eneo la Buza, wilaya ya Temeke, mshtakiwa alikutwa na vipande hivyo vya meno ya tembo, mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika shtaka la nne, ambalo ni kujihusisha na biashara ya meno ya tembo, linalowakabili washtakiwa wote, inadaiwa kati ya Novemba Mosi na Novemba 21, 2018, washtakiwa hao walisafirisha vipande 18 vya meno ya tembo kutoka Lindi kuja Dar es Salaam, bila kuwa na kibali.

Katika shtaka la tano tarehe hiyo hiyo washtakiwa wote kwa pamoja walitakatisha fedha huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz