Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Washtakiwa mauaji ya Dk Mvungi wapata hakimu mpya

Washtakiwa mauaji ya Dk Mvungi wapata hakimu mpya

Mon, 10 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Washtakiwa sita katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mjumbe wa tume ya mabadiliko ya katiba, Dk Sengondo Mvungi wamepata hakimu mwingine baada ya kumkataa wa awali.

Kwa nyakati tofauti washtakiwa hao wamekuwa wakiwakataa mahakimu kwa madai ya kutokuwa na imani nao.

Kesi hiyo sasa imehamishiwa kwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Huruma Shaidi. Awali kesi hiyo ilikuwa kwa Hakimu Mwandamizi Augustina Mmbando ambaye walimkataa.

Baadaye shauri hilo lilihamishiwa kwa Hakimu Augustine Rwezile ambaye kwa sasa ni Jaji na kesi hiyo kuhamishiwa kwa  Hakimu mwandamizi, Vicky Mwaikambo ambaye walimkataa pia.

Leo Jumatatu Februari 10, 2020 wakili wa Serikali, Groly Mwenda amedai kuwa amepewa taarifa kesi hiyo imehamishiwa kwa Hakimu Shaidi, kwamba hana jalada la shauri hilo hana ameiomba Mahakama hiyo kuahirisha  shauri hilo aweze kufuatilia kesi hiyo imefika kwenye hatua gani.

"Nimepewa taarifa leo kuwa kesi hii imehamishiwa kwa Hakimu Shaidi hivyo  sina jalada naiomba mahakama hii ipange tarehe nyingine ili shauri hili litakapokuja tena nitaieleza mahakama hii imefikia  hatua gani," amedai Mwenda.

Pia Soma

Advertisement

 

 Baada ya maelezo hayo mshtakiwa Longishu Losindo alinyoosha mkono na kuieleza mahakama hiyo kuwa shauri ni la muda mrefu kila linapokuja wakili wa Serikali amekuwa akidai kuwa upelelezi haujakamilika.

Hakimu Shaidi amesema anashindwa kumuuliza wakili wa Serikali kuhusiana na madai waliyowasilisha kwa kuwa jalada hana na kuwataka wasubiri hadi tarehe ijayo atakapoieleza mahakama hiyo shauri hilo limefikia kwenye hatua gani.

Mbali na Losindo wengine ni Msigwa Matonya, Mianda Mlewa, Paulo Mdonondo, Juma Kangungu na John Mayunga.

Katika kesi ya msingi washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka la mauaji inadaiwa kuwa Novemba 3, 2013 walifanya kosa la mauaji ya kukusudia kinyume na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 .

Inadaiwa siku hiyo ya tukio katika eneo la Msakuzi Kiswegere lililoko eneo la Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja walimuua Dk Mvungi kwa kukusudia.

Chanzo: mwananchi.co.tz