Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Washtakiwa kesi ya mauaji Mtwara wamkana wakili

Mauaji Polisi Mtwara Washtakiwa kesi ya mauaji Mtwara wamkana wakili

Fri, 11 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Washtakiwa saba wa kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini ambao ni maofisa wa polisi mkoani hapa, wamesema hawakuwahi kuingia mkataba na wakili yeyote wa utetezi, ila muda mwafaka ukifika watafanya hivyo.

Washtakiwa hao walieleza hayo katika Mahakama ya Hakimu mkazi Mtwara juzi ambapo kesi hiyo ilifika kwa ajili ya kutajwa, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Makahama hiyo, Lugano Kasebele.

Mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, aliyekuwa Mkuu wa upelelezi Wilaya ya Mtwara, Gilbert Kalanje aliieleza Mahakama hiyo kuwa yeye binafsi hajawahi kuingia mkataba na wakili yeyote.

“Mheshimiwa hakimu katika kumbukumbu zako naomba ieleweke kwamba mimi kama mshtakiwa namba moja, sijawahi kuingia mkataba wala kuongea na wakili yeyote, ikifika muda mwafaka nitafanya hivyo, vilevile tunaomba tupatiwe hati ya mashtaka,” alisema Kalanje.

Mara baada ya kusema hivyo, washtakiwa wengine wote nao waliieleza Mahakama hiyo kuwa hawajawahi kuingia mkataba na wakili yeyote.

Kalanje alitoa ufafanuzi huo mara baada ya hakimu Kasebele kuaihirisha kesi hiyo hadi Machi 22, 2022 itakapotajwa tena.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuahirisha kesi hiyo, Hakimu Kasebele alisema kauli ya washtakiwa hao imeisaidia Mahakama kujua kuwa hawakuwahi kuwa na wakili yeyote.

Februari 22, 2022 mahakamani hapo wakili Issa Chiputula wa kampuni ya Phoenix alijitambulisha kuwa yeye ndiye anayewawakilisha washtakiwa hao wote.

Mwananchi lilipomtafuta wakili Chiputula aliahidi kurudi kwa mwandishi muda si mrefu, lakini baada ya hapo hakupokea tena simu.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Januari 25, 2022 kwa shtaka la mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Musa Hamis.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live