Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Washtakiwa kesi ya dhahabu wahukumiwa

49074 Washtakiwapic

Thu, 28 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Serikali huenda ikakusanya zaidi ya Sh529.8 milioni iwapo washtakiwa wanne kati ya 12 wa kesi ya jinai namba 1/2019 ya kusafirisha shehena ya dhahabu kilo 323.6 zenye tahamani ya Sh27.18 bilioni na fedha taslimu Sh305 milioni watalipa faini kuepuka kifungo cha miaka 15 jela walichopewa baada ya kutiwa hatiani.

Akitoa hukumu baada ya washtakiwa kukiri makosa yao leo Machi 27, 2019, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Rhodha Ngimilanga aliwahukumu washtakiwa kwenda jela kati ya miaka mitano hadi 15 au kulipa faini kati ya Sh5milioni hadi Sh100 milioni.

Waliohukumiwa adhabu hiyo ni wafanyabiashara Hassan Sadiq, Emmanuel Mtemi, Kisabo Nkinda na Sajid Hassan waliokuwa wakitetewa na mawakili Emmanuel Safari na Michael Nasimile.

Pamoja na hukumu ya kifungo kwa muda tofauti na faini kulingana na makosa, Mahakama pia imeamuru kutaifishwa kwa kilo 319 za dhahabu, fedha taslimu Sh305 milioni, magari mawili, kilo sita za madini ya vito na mashine ya kupima ubora wa madini.

Katika hukumu yake, Hakimu Ngimilanga aliwatia hatiani washtakiwa katika mashtaka sita ambapo kwa shtaka la kwanza washtakiwa wote wanne wamehukumiwa faini Sh5 milioni au kifungo cha miaka 15 jela.

Katika shtaka la tatu Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa wa kwanza, Hassan Sadiq na kumhukumu kulipa faini Sh5 milioni au kwenda jela miaka 15.

Related Content

Washtakiwa wote wanne pia wametiwa hatiani katika kosa la tano na kuhumiwa kulipa faini Sh600, 000 kila mmoja au kifungo jela miaka mitano.

Mahakama pia imewahukumu washtakiwa kulipa faini ya Sh600,000 kila mmoja au kifungo cha miaka mitano jela.

Mshtakiwa Hassan Sadiq pia ametiwa hatiani katika shtaka la nane na kuhukumiwa adhabu ya faini Sh5 milioni au kwenda gerezani miaka mitano.

Katika shtaka la tisa, washtakiwa wote kila mmoja amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya Sh5 milioni.

Wakati wenzao wanne wakikiri makosa na kuhukumiwa, washtakiwa wengine wanane, wote wakiwa ni waliokuwa askari polisi akiwemo aliyekuwa mkuu wa operesheni mkoa wa Mwanza, Morice Okinda walikana mashataka na kurejeshwa rumande hadi Aprili 10, kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa baada ya upelelezi kukamilika.

Wengine wanaoendelea na kesi ni E. 6948 D/CPL. Kasala, F. 1331 PL. Matete, G. 6885 D/C Alex, G. 5080 D/C Maingu, G. 7244 D/C Timothy, G. 1876 D/C Japhet na H. 4060 D/C David Kadama.

Washtakiwa hao walikamatwa kati ya Januari 4 na 5, 2019 wakisafirisha shehena ya dhahabu na fedha taslimu Sh305 milioni kinyume cha sheria.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa walifikishwa mahakamani Januari 11, 2019 na kusomewa mashtaka 12 kabla ya hati mashtaka kubadilishwa na kubakisha mashtaka 10 ikiwemo kuomba na kupokea rushwa, kuongoza uhalifu, kutakatisha fedha, kukutwa na madini kinyume cha sheria na kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Tukio la kukamatwa kwa shehena hiyo ya dhahabu na mamilioni ya fedha taslim lilifanikiwa baada ya vyombo vya dola kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Akizungumzia tukio hilo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kuwaapisha viongozi wapya aliowateua, Rais John Magufuli alisema askari polisi waliokamatwa walikuwa wakiwasindikiza watuhumiwa kutoka jijini Mwanza kwenda Geita kupokea sehemu ya rushwa ya zaidi ya Sh300 milioni baada ya kupokea Sh700 milioni kati ya Sh1 bilioni waliyokubaliana.

Katika maelezo yake, Rais Magufuli alisema mchezo wao uliposhtukiwa, askari hao walijifanya kupiga king’ora wakijidai nao walikuwa wakiwafuatilia watuhumiwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz