Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Washtakiwa kesi ya Luck Vincent kusuka, kunyoa leo

61605 KESISHULEPIC

Fri, 7 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakazi wa jijini Arusha na maeneo ya jirani wanatarajiwa kujitokeza mahakamani kusikiliza hukumu ya kesi inayowakabili mmiliki wa Shule ya Lucky Vicent, Innocent Moshi na mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo, Longino Vicent (40) kutokana na ajali ya gari iliyotokea Mei 6, 2017 na kuangamiza watoto 32, walimu wawili na dereva mmoja.

Ajali hiyo, ilitokea Mei 6, 2017, katika eneo la Rhotia wakati, wanafunzi wa shule hiyo, wakitoka Arusha majira ya saa 12 asubuhi kwenda wilayani Karatu, katika mitihani ya ujirani mwema katika Shule ya Tumaini Academy.

Katika kesi hiyo, washitakiwa wanakabiliwa na jumla ya mashitaka matano ya kuvunja sheria za usalama barabarani, ikiwemo kuendesha gari za abiria bila kuwa na leseni ya usafirishaji, gari lililosababisha ajali kutokuwa na bima, kushindwa kuingia mkataba baina ya dereva na mwajiri na kosa la kuzidisha abiria 13 katika gari lililopata ajali ambalo linamkabili mwalimu mkuu msaidizi.

Moshi aliieleza mahakama Mei 9, 2017, alikamatwa na polisi na kuwekwa ndani kwa sababu ya ajali hiyo na baada ya siku tatu alipelekwa mahakamani na moja ya makosa aliyoshitakiwa ni kosa la kuendesha gari bila kuwa na leseni  ya biashara.

Alisema pia alishitakiwa kwa kosa la kutumia gari bila kuwa na bima na kuwapakia wanafunzi  38 ndani ya basi dogo kinyume na sheria kwani linapaswa kubeba abiria 25.

Alisema kuwa yeye hajatenda makosa hayo pia kampuni ya Lucky Vincent iliuziwa gari na Swalehe Kiluvia na kuwakabidhi kadi ya gari, bima ya gari na leseni ya gari hilo.

Pia Soma

Mshitakiwa wa  pili mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo, Longino Vicent (40) aliieleza mahakama kuwa Mei 6, 2017, alifika shuleni saa 12 asubuhi na kushughulikia zoezi la usafiri wa wanafunzi aliopewa na mwalimu mkuu na gari tatu za kwenda Karatu.

Vicent alikanusha kuhusika na ajali hiyo kwani hakuwepo eneo la tukio na yeye alitimiza wajibu aliokabidhiwa na mkuu wa shule kuwasafirisha wanafunzi hao wakiwa na walimu wao.

Ajali hiyo ilizua hisia za simanzi jijini Arusha na duniani kote huku Serikali na wadau mbalimbali wakijitolea kuwasaidia walioathiriwa wakiwemo walionusurika, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa.

Katika kumbukumbu ya mwaka mmoja ya ajali hiyo, mamia ya watu walihudhuria kumbu kumbu hiyo iliyoanza kwa ibada na baadaye hotuba mbalimbali pamoja na kuweka mashada ya maua katika mnara wa kumbukumbu uliojengwa katika shule hiyo.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz