Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Washtakiwa kesi ya Dk. Mvungi wasomewa tena mashtaka

WAUAI MVUNGI Washtakiwa kesi ya Dk. Mvungi wasomewa tena mashtaka

Tue, 12 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

JAMHURI kwa mara nyingine imewasomea maelezo ya ushahidi washtakiwa wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi.

Washtakiwa walisomewa maelezo ya mashahidi jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Wakili wa Serikali, Anna Chimpaye aliwataja washtakiwa kuwa ni Msigwa Matonya, Mianda Mlewa, Paulo Mdonondo, Juma Kangungu, Longishu Losingo na John Mayunga.

Upande wa mashtaka utakuwa na mashahidi 33 na vielelezo 18 wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo Mahakama Kuu.

Alitaja miongoni mwa vielelezo hivyo kuwa ni cheti cha kifo, ripoti kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na ramani ya tukio.

Alidai miongoni mwa mashahidi hao, ni Ally Abdalah mjumbe wa shina namba 33 eneo la Kiwalani Migombani.

Akisoma maelezo ya shahidi huyo, alidai Novemba 12, 2013, akiwa nyumbani kwake walifika watu watano wakitaka kufanya upekuzi katika nyumba ya Mayunge maarufu Ngosha.

Alidai kuwa katika upekuzi huo, walikuta bastola ndogo aina ya Revolva, risasi 21 na baruti nne zilizokuwa ndani ya mfuko wa nailoni zilizofichwa ndani ya nyumba hiyo juu ya paa la nyumba pembeni.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia ambapo inadaiwa Novemba 3, 2013, kinyume na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 walitenda kosa hilo.

Ilidaiwa siku ya tukio eneo la Msakuzi Kibwegere, Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja walimuua kwa kukusudia Dk. Sengondo Mvungi.

Desemba 22, 2013, washtakiwa hao na wengine walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka ya mauaji.

Upelelezi wa kesi hiyo ulipokamilika washtakiwa wanne waliachiwa huru, jalada likahamia Mahakama Kuu kwa kesi kuanza kusikilizwa.

Novemba 22, 2018, wakati kesi hiyo inataka kuanza kusikilizwa DPP aliwasilisha hati akionyesha hana nia ya kuendelea na shauri hilo, washtakiwa wakaachiwa huru.

Muda mfupi baada ya kuachiwa walikamatwa tena na kusomewa upya mashtaka hayohayo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo jana wamesomewa maelezo ya mashahidi ili kesi ihamie Mahakama Kuu kwa kusikilizwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live