Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Washtakiwa 39 wa ugaidi waachiwa kwa dhamana

Rama Washtakiwa 39 wa ugaidi waachiwa kwa dhamana

Mon, 28 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama kanda ya Mwanza imewaachia kwa dhamana washtakiwa 39 wa ugaidi ambao wametakiwa kuripoti polisi mara mbili kwa mwezi kwa miaka mitatu mfululizo.

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ililiridhia washtakiwa hao kuachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi vigezo na kutakiwa kuendelea kuripoti polisi.

 Kadhalika, Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia mchungaji Diana Bundala wa kanisa la Zumaridi lililoko jijini Mwanza kwa kosa la kufanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Mwanza, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Ramadhani Ng'anzi, alisema mahakama imeagiza washtakiwa hao kuripoti ofisi ya DPP mara mbili kwa mwezi mfululizo kwa miaka mitatu.

Ng'anzi alisema washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na makosa mbalimbali yanayohusiana na ugaidi mkoani humo na kwa sasa wameachiwa kwa dhamana.

Alipoulizwa kama washtakiwa hao wapo wanasiasa, hakuwa tayari kutoa majibu ya moja kwa moja na badala yake akaeleza kwamba sheria haiangalii ukubwa wa nafasi ya mtu alionao.

“Hapa hatuangalii kama ni mwanasiasa,  sheikh ama mtu kwa nafasi aliyonayo bali tunaangalia suala la sheria za nchi zinasemaje,'' alisema.

Akizungumzia sakata la mchungaji kufanya biashara haramu, Kamanda Ng'anzi alisema, mtuhumiwa alikamatwa nyumbani kwake  akiwa na idadi ya watu  149  wanaoishi kwake.

Mchungaji huyo mwenye umri wa miaka 39,  mkazi wa Mtaa wa Buguku Buhongwa, anatuhumiwa kuhusika na usafirishaji haramu wa binadamu wapatao 149.

Alisema chanzo cha kukamatwa na kubainika biashara hiyo haramu ni kutokana na mwanamke mmoja kwenda kujificha kwa mchungaji huyo akijaribu kumficha mtoto asiende shule.

Awali Mahakama ya Mwanzo ya Mkuyuni jijini  Mwanza ilitoa amri kwa Jeshi la Polisi kumkamata mzazi wa kike wa mtoto, Samir Ally Abbas, ayetakiwa kufikishwa mbele ya mahakama hiyo baada ya kesi ya msingi kusikilizwa.

Kutokana na ukatili huo, mahakama iliagiza Jeshi la Polisi kwenda kumsaka mwanamke huyo pamoja na mtoto wake ambaye ni mwanafunzi.

''Siku ya kwanza askari wetu walienda nyumbani kwa mchungaji huyo,  lakini kwa kuwa walikuwa wachache walishindwa kuwakamata mchungaji na watuhumiwa wengine,  hivyo askari wetu wakarudi na siku ya pili waliongeza nguvu na kufaninikiwa  kuwakamata watuhumiwa hao,'' alisema Kamanda  Ng'anzi.

Alisema baada ya askari kuingia nyumbani kwa mchungaji huyo, walikuta idadi kubwa  ya watu na walipofanya uchunguzi walibaini mtuhumiwa huyo alikuwa  akifanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu.

Aliongeza kuwa watu hao wametolewa mikoa mbalimbali  kisha mchungaji huyo kuwafungia nyumbani kwake kwa lengo la kuwatumikisha na kati yao wanaume 57, wanawake 92.

Katika idadi hiyo wapo watoto 24, wanaokadiriwa kuwa na miaka kati ya 4 hadi 17, ambao wamekatizwa masomo kinyume cha sheria.

Kamanda aliongeza kuwa mchungaji huyo alikuwa akiwaaminisha watu hao kwamba yeye ni Mungu anayeponya, kufufua wafu na kutatua matatizo yao.

Ng'anzi alisema serikali iliwahi kufuta kibali cha kuanzishwa kanisa hilo na kwamba mchungaji huyo alikuwa akifanya kazi za uchungaji bila kibali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live