Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapandishwa kortini mashitaka 746, yamo kughushi, utakatishaji

F7c961a4a13b982e0f397ba82874dcf8 Washtakiwa wakiwa Mahakamani

Wed, 30 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu tisa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam leo wakikabiliwa na mashitaka 746 ikiwemo kughushi na kutakatisha fedha haramu zaidi ya Sh bilioni 4.7, mali ya benki ya NBC tawi la Mnazi Mmoja, Ilala, Dar es Salaam.

Washitakiwa hao ni Baraka Madafu, Mark Mposo, Lusekelo Mbwele, Leena Joseph, Bernard Mndolwa, Salvina Karugaba, Mohamed Kombo, Hussein Amani na Paul Shayo ambaye alienda kusomewa mashtaka katika hospitali ya Kitengule Tegeta alikolazwa.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Faraji Nguka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ritha Tarimo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na Nguka, ilidaiwa kuwa shtaka la kwanza linalowakabili washtakiwa wote ni kuongoza genge la uhalifu na kujipatia kiasi cha Sh 4,786,800,000 kosa wanalodaiwa kulitenda kati ya Aprili 1, 2019 na Desemba 31, 2020 katika Benki ya NBC tawi la Mnazi Mmoja, Ilala Dar es Salaam.

Katika shtaka la pili ilidaiwa kuwa katika tarehe hizo na maeneo hayo washtakiwa hao walisababishia hasara kwa mamlaka, ambapo ilidaiwa kuwa kwa nia ovu waliisababishia hasara ya kiasi hicho cha fedha benki ya NBC tawi la Mnazi Mmoja.

Katika shtaka la tatu la utakatishaji fedha haramu ilidaiwa kuwa katika tarehe hizo na maeneo yaliyotajwa awali, washtakiwa hao walijipatia kiasi hicho cha fedha huku wakijua kuwa ni zao la kosa tanguli la kughushi.

Nguka aliendelea kudai kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa pia na mashtaka 371 ya kughushi nyaraka na mengine 371 ya kuwasilisha nyaraka za uongo makosa ambayo waliyafanya katika tarehe hizo hizo na maeneo hayo.

Nguka alidai upelelezi wa kesi hiyo uko katika hatua za mwisho na wako katika mchakato wa kufungua jalada katika Mahakama Kuu, ili kuendelea na hatua nyingine za kusikilizwa.

Pia Wakili Nguka aliomba mahakama hiyo ihamie katika hospitali ya Kitengule eneo la Tegeta, ambako mshtakiwa Paul Shayo amelazwa, ili akasomewe mashtaka yake akiwa hospitalini hapo, hoja ambayo ilikubaliwa na kutekelezwa.

Baada ya kusomwa mashtaka hayo Hakimu Tarimo aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 13, 2022 na washtakiwa wote walipelekwa mahabusu kwa kuwa shtaka la takatishaji fedha haramu halina dhamana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live