Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapandishwa kizimbani kwa madai ya kukutwa na tausi wa Ikulu

81745 Tausi+pic Wapandishwa kizimbani kwa madai ya kukutwa na tausi wa Ikulu

Sat, 26 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watu watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu wakikabiliwa na mashtaka matano likiwemo la  kukutwa na ndege watatu aina ya tausi waliokuwa Ikulu wenye thamani ya zaidi ya Sh3.4milioni.

Washtakiwa hao wanaokabiliwa na kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 116/2019 ni David Graha, Mohamed Hatibu na Mohamed Ally.

Leo Ijumaa Oktoba 25, 2019 wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo amedai washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la  kuongoza mtandao wa uhalifu, kukutwa na nyara za Serikali, kukutwa na mali bila ya kuwa na kibali na utakatishaji fedha.

Nchimbi amedai kati ya Juni Mosi, 2015 na Oktoba 4, 2019 jijini Dar es Salaam washtakiwa hao waliratibu mpango wa kujihusisha na ndege aina ya tausi bila ya kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.

Katika shtaka la pili katika tarehe hiyo jijini Dar es Salaam wote kwa pamoja walikutwa na ndege hao mali ya Tanzania huku wakiwa hawana kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori.

Katika shtaka la tatu wanadaiwa Oktoba 14, 2019 maeneo ya Mikocheni mshtakiwa Hatibu alikutwa akimiliki ndege hao bila ya kuwa na kibali.

Pia Soma

Advertisement
Katika shtaka la nne kati ya Juni Mosi, 2015 na Oktoba 14, 2019 jijini Dar es Salaam mshtakiwa Graha na Hatibu walijipatia Sh300,000 huku wakijua ni mazalia ya kosa tangulizi.

Shtaka la mwisho wanadaiwa kati ya  Juni Mosi, 2015 na Oktoba 14, 2019 jijini Dar es Salaam walishirikiana na kujipatia Sh300,000 huku wakijua fedha hizo ni mazalia kosa tangulizi.

Baada ya Nchimbi kusoma hati ya mashtaka alieleza kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine.

Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 7, 2019 itakapotajwa tena.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz