Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waomba shahidi aitwe tena kesi vigogo CWT

Kisutu12 660x400 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

Thu, 10 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Upande wa mashitaka katika kesi inayowakabili aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif na mweka hazina wake, Abubakar Allawi umeiomba mahakama kumuita tena mahakamani shahidi wa tano, Moses Mnyazi ili aieleze mahakama zilipo nyaraka halisi zilizotumika kuwalipa posho ya safari ya kwenda Cape Verde washitakiwa hao.

Hayo yalijiri jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi anayesikiliza kesi hiyo.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kujipatia Sh milioni 13.9, mali ya chama hicho isivyo halali.

Akiwasilisha ombi hilo, wakili wa serikali kutoka Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Imani Mitume alidai shahidi huyo ndiye alipewa nyaraka halisi na Seif ili azifanyie kazi.

Alidai, hata hivyo Seif wakati akihojiwa alisema hajui zilipo nyaraka hizo ingawa kumbukumbu za mahakama zinaonesha kuwa Mnyazi ndiye aliyefanyia kazi nyaraka hizo hivyo akaomba aitwe tena mahakamani.

Akijibu hoja hiyo wakili wa utetezi, Nesto Mkoba alipinga ombi hilo na kudai kuwa shahidi huyo alishatoa ushahidi kuhusu vielelezo hivyo, hivyo akaiomba mahakama kutotilia umuhimu hoja hiyo. "Imani yetu ni kwamba upande wa mashitaka wanataka kucheleweshwa kesi kwani shahidi huyo alishapewa nafasi na akaja kutoa ushahidi kuhusu vielelezo hivyo.

Mahakama hii ilishatoa uamuzi mara mbili kuhusiana na vielelezo hivyo, naomba ombi hili liondolewe," alidai.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote Hakimu Kyaruzi aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 9, 2022 kwa ajili ya kutoa uamuzi Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa kati ya Oktoba 3, 2018 na Novemba 6, 2018, katika Ofisi za CWT zilizopo Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa waajiriwa wa chama hicho, walitumia Mamlaka yao vibaya. kwa kujipatia Sh 13,930,693. Washtakiwa hao pia wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya na kwa manufaa yao kuchepusha fedha hizo ambazo ni mali ya CWT.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live