Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanne wauawa kwa mapanga mgodini

CRIME SCENE.png Wanne wauawa kwa mapanga mgodini

Wed, 1 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAFANYAKAZI wanne wa kiwanda cha uchenjuaji madini ya dhahabu (Plant) katika mgodi mdogo wa Ntambalale, kijiji cha Wisolele, wilayani Kahama wameuawa kwa kucharangwa na mapanga na watu wasiojulikana na kutokomea.

Mwenyekiti wa mgodi huo, Hamisi Mabubu, akiongea na Nipashe kwa njia ya simu, alisema tukio hilo limetokea saa tisa usiku wa kuamkia jana katika moja ya kiwanda cha uchenjuaji wa madini mgodini hapo.

Alisema, wafanyakazi watano wa kiwanda hicho, walivamiwa na kucharangwa mapanga na watu wasiojulikana na kuibia kaboni, huku wanne kati ya hao wakipoteza maisha papo hapo na mmoja Evvary Mbuya, akijeruhiwa.

Mabubu alisema, chanzo cha tukio hilo ni tamaa ya kupata mali kwa haraka, na kudai mwanzo wa mwezi huu pia kulitokea uvamizi kwenye kiwanda cha uchenjauji wa madini na kuiba kaboni, lakini hawakujeruhi mtu.

Diwani wa Kata ya Segese, Joseph Mayala, alisema alipata taarifa ya tukio hilo kutoka kwa mtendaji wake wa kata majira ya saa 10 usiku na walipofika kwenye tukio walikuta miili ya wafanyakazi wa kiwanda hicho ikiwa imehifadhiwa kwenye chumba kimoja cha kiwanda hicho.

Alisema, wakiwa katika harakati za kuwaondoa katika chumba hicho, waligundua mmoja wao ambaye ni Mbuya akiwa bado hai na kumkimbiza Hospitali ya Halmashauri ya mji wa Kahama kwa ajili ya matibabu zaidi.

Mayala alisema, tukio la uvamizi wa kiwanda cha uchenjuaji wa dhahabu sio la kwanza, na hutokea wakati wamiliki wa viwanda wakiwa na kaboni na kuliomba Jeshi la Polisi kuongeza ulinzi na kudhibiti majanga hayo yasiendelee kutokea.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, ACP Joseph Paul, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na harakati za kuwatafuta na kuwatia nguvuni walitotenda tukio hilo zinaendelea ili wafikishwe katika vyombo vya sheria.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live