Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanne wanaswa na 'unga' JNIA

08e1e58c531eaf131af1c71f15c56b85 Wanne wanaswa na 'unga' JNIA

Wed, 13 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshila Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege Tanzania limewakamata watuhumiwa wanne kwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege Tanzania, Jeremia Shila akizungumza na waandishi wa habari jana alisema dawa zilizokamatwa ni methamhetamine, kokeini, bangi na heroine.

Dawa hizo zilikamatwa kati ya Machi 17 hadi Aprili 8, mwaka huu.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, dawa hizo ziliwekwa katika chaji za simu na nyingine zilimezwa na mmoja wa watuhumiwa.

“Majira ya 11:00 asubuhi Machi 17, 2022 katika eneo la ukaguzi la Kampuni ya Kusafirisha Vifurushi ya DHL, Polisi kwa kushirikiana na maofisa wa DHL tulikamata kifurushi kimoja kikiwa na chaja saba za kuchajia simu ambazo sita kati ya hizo zilikuwa na unga mweupe wenye uzito gramu 234.54 wa dawa za kulevya aina ya methamphetamine,” alisema Kamanda Shila na kuongeza kuwa kifurushi hicho kilitumwa toka Johannesburg nchini Afrika Kusini kwenda Singida.

Alisema kwa kushirikiana na Polisi mkoani Singida, wamemkamata raia wa China mwenye umri wa miaka 35 na tayari jalada la mashtaka limefikishwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua za kisheria. Mchina huyo ndiye aliyekuwa akitumiwa mzigo huo.

Pamoja na kifurushi hicho, Aprili 4, mwaka huu saa 7:00 mchana eneo la abiria wanaowasili walimkamata mkazi wa Kitunda aliyewasili nchini na Shirika la Ndege la Ethiopia akitokea Delhi nchini India kupitia Addis Ababa, Ethiopia akiwa amemeza pipi mbili za dawa za kulevya aina ya kokeini.

Aliongeza kuwa Aprili 7, mwaka huu saa 12:30 mchana katika Jengo la Tatu la Abiria walimkamata mkazi wa Tabata mwenye hati ya kusafiria namba TAE 445026 aliyekuwa akisafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates kwenda Istanbul, Uturuki akiwa na dawa za kulevya aina ya bangi.

Pia Aprili 8, mwaka huu saa 20:30 usiku katika Jengo la Tatu la Abiria alikamatwa mtuhumiwa mwingine aliyekuwa akisafiri kwenda Paris, Ufaransa kupitia Nairobi na Amsterdam kwa Shirika la Ndege la Kenya, akiwa na dawa za kulevya aina ya heroine alizoficha kwenye kitako cha begi lake la nguo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live