Washtakiwa wanne kati ya watano wanaodaiwa kumuua Milembe Suleman (43), wamekutwa na kesi ya kujibu na wataanza kujitetea kesho Juni 28, 2024.
Akitoa uamuzi baada ya upande wa Jamhuri kuomba kufunga ushahidi wake kutoka kwa mashahidi 29 na vielezo 19, Jaji wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina amesema kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa, washtakiwa wanne wamekutwa na kesi ya kujibu.
Washtakiwa hao wanashtakiwa kwa kosa moja la mauji kinyume na kifungu cha 196&197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, kosa wanalotuhumiwa kulitenda Aprili 26, 2023 kwa kumkata Milembe na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili.
Waliokutwa na kesi ya kujibu ni Dayfath Maunga (30), Safari Labingo (54), Genja Pastoy na Musa Pastory na kutakiwa kujitetea chini ya kifungu cha 293(1)2ab kuanzia kesho.
Kuhusu mshtakiwa wa tano, Ceslia Macheni, Jaji Mhina amesema ushahidi na vielelezo vyote vilivyotolewa hakuna kinachomuunganisha na kosa analoshtakiwa nalo na kupitia ushahidi na vielelzo vilivyotolewa hakuna kinachoonyesha kama alipanga au kutekeleza kosa hilo.
Pamoja na hayo, amesema ushahidi uliotolewa hauonyeshi kama mshtakiwa huyo alikuwa na ufahamu wowote kabla na baada ya tukio la mauaji.
Kitu pekee kinachomuunganisha na shtaka hilo, amesema ni ushahidi wa shahidi aliyemkamata mshtakiwa wa tatu, kuwa yeye (mtuhumiwa) akiwa kama mganga wa kienyeji, watuhumiwa walienda kwake kwa ajili ya kuoshwa.
Amesema mashahidi hao hawakueleza kama mshtakiwa aliambiwa au alikuwa na ufahamu kama watu hao walikuwa wametenda kosa la mauaji na hivyo, mahakama ikamwachia huru.
Awali, kabla ya kutoa uamuzi huo, mahakama ilipokea vielelezo viwili, jambia linalodaiwa kutumika kumkatakata Milembe na kusababishia kifo chake na fomu ya upekuzi ya eneo lilikokuwa limefichwa jambia, eneo la Mwatulole mjini Geita.
Akitoa ushahidi wake, shahidi wa 28 ambaye ni mpelelezi wa kesi hiyo, Pascal Mwinamila ameieleza mahakama kuwa baada ya kupewa maelekezo ya kupeleleza tukio hilo, alikwenda eneo yalikotokea mauji na kwenye nyumba ya kulala wageni ya Calfonia, alikokuwa akilala Milembe na kuchukua picha cha CCTV za Aprili 25, 2023.
Akiongozwa na mwendesha mashtaka, Merito Ukongoji, shahidi huyo amedai kuwa Mei 6, 2023 alizungumza na mshtakiwa wa tatu, Genja Pastory aliyemweleza alikoficha jambia na baada ya kulipata, walikuta likiwa na damu kwenye makali na kwenye mshikio.
“Nikiwa na askari wengine, tulitafuta jambia na tulipolipata, kwa juu kwenye makali lilikiwa na meno kama msumeno likiwa limechafuka damu kwenye makali na kwenye mshikio kwa juu,” amedai Mwinamila.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, Mei 7,2023 akiwa na askari wenzake, alimchukua mshtakiwa wa tatu, Genja Pastory kwenda kuwaonyesha walikotupa simu za marehemu baada ya kumuua.
Akizungumzia uhusika wa washtakiwa wote watano katika kesi hiyo, shahidi huyo amedai kuwa mshtakiwa wa kwanza, Dayfath Maunga ndiye alianza taratibu za kuzungumza na Safari Lubingo (mshtakiwa wa pili) na kula njama za kumuua Milembe Suleman.
Amedai kuwa uhusika wa mshtakiwa wa pili unatokana na mazungumzo aliyofanya na mshtakiwa wa kwanza na kufanya mpango wa kuwapata watu waliohusika kumuua Milembe, Safari Lubingo aliwasiliana na Musa Pastory na Genja Pastory.
Shahidi huyo amedai baada ya washtakiwa Genja na Musa kushindwa kumuua Milembe wakiwa nyumba ya wageni ya Kisesa, walirudi nyumbani na Genja alifanya mazungumzo tena na Safari na kumtaka awatafutie watu wengine kwa kuwa Musa haonyeshi nia ya kuendelea na kazi hiyo.
Amedai baada ya hapo, Safari alimtafuta mtu aitwaye Masumbuko na Buchuchu ambao kwa pamoja walikutana na mshtakiwa wa kwanza, Dayfath na kukubaliana kufanya kazi hiyo kwa ujira wa Sh2.6 milioni zilizolipwa kwa awamu.
Mwinamila ameieleza mahakama kuwa baada ya Genja na wenzake kutekeleza mauaji ya Milembe, walikwenda nyumbani kwa mshtakiwa wa tano, Cecilia Macheni aliyekuwa mganga wa kienyeji kwa ajili ya kuoga dawa na kuondoa mkosi.
Washtakiwa hao wanatetewa na mawakili, Liberatus John (mshtakiwa wa kwanza), Laurent Bugoti anayemtetea mshtakiwa wa pili, Elizabeth Msechu anayemtetea mshtakiwa wa tatu, Erick Lutehanga na Yesse Lubunda aliyekuwa akimtetea mshtakiwa wa tano.
Kesi hiyo itaendelea kesho Ijumaa Juni 28, 2024 kwa washtakiwa kuanza kujitetea.