Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanne wahukumiwa kunyongwa kwa kumuua mwanafunzi

6d42aea3ad934256335c9c4b90effad3.jpeg Washitakiwa hao walimuua mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nzega

Tue, 3 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, imewahukumu wakazi wanne wa Nzega mjini wanyongwe hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kosa la mauaji.

Akitoa hukumu hiyo katika kikao cha mahakama kuu kinachoendelea wilayani Nzega mkoani Tabora, Jaji Mfawidhi wa mahakama kuu kanda hiyo, Amor Khamis alisema kutokana na ushahidi usioacha shaka uliotolewa mahakamani, mahakama imewakuta na hatia ya kuua.

Awali, Wakili wa Serikali kutoka ofisi ya taifa ya mashitaka wilayani Nzega, ukiongozwa na Jenifa Mandago waliieleza mahakama kuwa kati ya Septemba 30 na Oktoba Mosi mwaka 2015, washitakiwa hao walimuua mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nzega, Hosamu Abdulhamani kwa kutumia kitu chenye ncha kali, wakatenganisha kichwa cha marehemu na kiwiliwili chake.

Alisema mauaji hayo yalifanyika katika eneo la Kijiji cha Silimka Kata ya Utwigu Wilaya ya Nzega na Mkoa wa Tabora. Aliwataja washitakiwa kuwa ni Samwel Maganga, Selemeni Saidi, Paulo Maganga na Juma Dorard. Wakili huyo alisema kichwa cha marehemu huyo waliondoka nacho na hakikupatikana hivyo marehemu alizikwa bila kichwa.

Mahakama baada ya kuridhika na upande wa ushahidi, iliwatia hatiani na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa wakazi hao wote wanne ambao walikuwa ni wakazi wa mtaa wa Uswilu uliopo Nzega Mjini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live