Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanne kizimbani kwa kukutwa na vipande 39 vya meno ya tembo

11116 Meno+pic.png TanzaniaWeb

Tue, 10 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watu wanne wakiwamo polisi jamii wa Mbezi Luis jijini hapa wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, baada ya kutuhumiwa kukutwa na meno ya tembo ya thamani ya Sh239.5 milioni.

Wakili wa Serikali, Faraja Nguka jana mbele ya hakimu Ally Salum alieleza kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 45 ya 2018.

Aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Juma Myali (35), Greyson Muhapa (wote polisi jamii) na Kefas Mlenzi, dereva na mkazi wa Mbezi Luis.

Alisema washtakiwa hao kwa pamoja Juni 28 katika eneo la Mbezi Wilaya ya Ubungo, wanadaiwa kukamatwa wakiwa na vipande 30 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola 105,000 za Marekani (Sh239.5 milioni), bila kibali cha mkurugenzi wa wanyama pori.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa hawakuruhusiwa kuzungumza chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi hiyo.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo hakimu Salum aliahirisha kesi hadi Julai 23.

Katika kesi nyingine ya uhujumu uchumi, Hassan Sangali (22) mkulima mkazi wa Pingalama Kongwa jijini Dodoma, alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na shtaka la kukamatwa akiwa na vipande tisa vya meno ya tembo.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa Juni 9 eneo la Kimara Wilaya ya Ubungo alikamatwa na vipande hivyo vyenye thamani ya Dola 30,000 za Marekani (Sh66.7 milioni) bila kibali.

Mshtakiwa hakutakiwa kujibu lolote na hakimu Salum aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 23.

Chanzo: mwananchi.co.tz