Dodoma. Jeshi la Polisi mkoani Dodoma nchini Tanzania limewakata na kuwafikisha mahakamani wanawake watano na mwanaume mmoja aliyekuwa akimnunua mmoja wao na wote kuhukumiwa kifungo jela.
Wakati watano wakihukumiwa kifungo cha miezi sita, mmoja amehukumiwa kifungo cha miezi mitatu baada ya kukiri kosa.
Akizungumza leo Jumatano Septemba 11, 2019 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amesema watu hao walikamatwa Septemba 8, 2019 katika operesheni zinazofanywa na polisi maeneo mbalimbali mjini Dodoma.
Kamanda Muroto amesema kitendo hicho ni kinyume na kifungu 176 (a) (f) (g) cha kanuni ya adhabu sura ya 16.
Amesema usiku katika mtaa wa Uhindini na Viwandani, waliwakamatwa wanawake watano wakifanya biashara ya ukahaba huku wakidaiwa kuhatarisha amani na utulivu katika mtaa huo.
Amebainisha kuwa mwanamke mmoja kati yao alikamatwa akifanya ngono na mwanaume huyo, wote wamehukumiwa kifungo na kuchapwa viboko vitatu kila mmoja.
Pia Soma
- Mali za Dangote, Bakhresa hatarini kupigwa mnada
- Watu 666 wajiua ndani ya miaka minne Tanzania
- Afya ya Ruwa’ichi yaimarika, aanza kula
Septemba 5, 2019 Muroto aliwaeleza waandishi wa habari kuwa polisi iliwafikisha mahakamani wanawake 15 na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita kila moja baada ya kupatikana na hatia ya kujiuza.
Alieleza kuwa ulifanyika msako Septemba 2, 2019 saa tatu usiku mtaa wa Uhindini na kuwakamatwa wanawake 15 wakifanya biashara ya ukahaba huku wakidaiwa kuhatarisha amani na utulivu katika mtaa huo.
Alisema wamepelekwa gereza la Isanga na kupokewa kwa ajili ya nguvu kazi, kwamba wataponda kokoto na kufanya kazi nyingine.
Aliwataja kuwa ni Suzana Onesmo (27), Mariam Omary (29), Maimuna Issa (38), Bhoke Chacha (30), Swaumu Bakari (26), Rahma Abdi (28), Magreth Humphrey (27), Wema Saidi (25), Jeniffer Wilson (33), Lydia Kilale (30), Manka Richard (21), Mwasuma Hassan (26), Angel Joseph (29), Zaina ramadhani (30) na Tatu Saidi (27).”