Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaume 341 waeleza wanavyopigwa na wake zao

95812145bdb51958bb28426fcbd0e977 Wanaume 341 waeleza wanavyopigwa na wake zao

Sat, 19 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WANAUME 341 kati ya watu 752 wamejitokeza katika huduma za mkono kwa mkono zinazotembea maarufu ‘One Stop Center Mobile’ kuelezea madhira wayapatayo yakiwamo ya kutelekezewa watoto, dharau na kupigwa na wake zao.

HabariLeo lilibaini hayo katika utoaji wa huduma za ‘one stop center mobile’ katika wilaya ya Kipolisi ya Chanika, Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyofanyika Novemba 25 hadi Desemba 10, 2020.

Ilibainika kuwa katika huduma hizo za siku mbili katika kata za Chanika, Pugu na Gongolamboto, wanaume walikuwa miongoni mwa watu waliokuwa kwenye misululu wakisubiri na kisha kupata huduma hizo zikiwamo za upimaji wa macho, kisukari, shinikizo la damu na unasihi kwa waathirika wa unyanyasaji na ukatili wa kijinsia ukiwamo dhidi ya wanawake na watoto.

Aidha, HabariLeo lilishuhudia huduma katika maeneo hayo zikienda sambamba na kuwafikishia watu elimu katika maeneo yao kupitia vipeperushi, matangazo na mazungumzo ya ana kwa ana kuhusu maana, aina, madhara, kutambua na namna ya kupambana na ukatili huo.

Zaidi ya wananchi 3,600 sawa na wastani wa watu 600 kwa siku, walifikiwa na elimu hiyo. Juzi na jana huduma hizo zilikuwa Segerea na leo zinaanza Buguruni, Dar es Salaam hadi kesho.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Janeth Magomi na Mwasisi na Mratibu wa One Stop Center katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Dk Christina Onyango, walisema kwa nyakati tofauti wakiwa Segerea kuwa, mafanikio hayo yametokana na kutolewa kwa elimu dhidi ya ukatili wa kijinsia.

“Polisi Ilala tuliona baada ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, tuje na mwendelezo kwa kutoa huduma ili waathirika baada ya kuelewa, sasa wachukue hatua na kufunguka ndiyo maana tunawasogezea huduma katika maeneo yao,” alisema Kamanda Magomi.

Onyango alisema, “kwetu haya ni mafanikio makubwa kwa zaidi ya asilimia 100 maana kama kwa miezi miwili au zaidi mnaweza msipate mwanaume hata mmoja anayelalamikia ukatili wa kijinsia, lakini hapa kwa siku sita tumepata wanaume 341 na elimu kufikia watu zaidi ya 3,600 kwa siku sita, ni mafanikio makubwa.”

Alisema katika vituo hivyo vya huduma zinazotembea, watu 752 wakiwamo watoto 60, wanawake wakiwa 411 na wanaume 341, walijitokeza kutafuta huduma zikiwamo za afya.

“Waliohitaji huduma za polisi walikuwa 300, huduma za wanasheria 225, huduma za ustawi wa jamii 112 na huduma za afya 106. Kwa afya, karibu asilimia 90, walitaka huduma za upimaji wa macho na miwani,” alisema.

Kwa mujibu wa Onyango, miongoni mwa wanaume waliojitokeza, wengine walilalamikia kupigwa na wake zao, ulevi wa kupindukia wa wake zao, kukosa uaminifu katika ndoa, wanawake kutelekeza watoto siku nzima bila huduma na wanawake hao kurudi nyumbani usiku wakiwa wamelewa na kutukana ovyo.

Kuhusu polisi na ustawi wa jamii, wengi hasa wanawake walieleza vitendo vya kupigwa, ubakaji hata katika ndoa, ulawiti na mateso dhidi ya watoto.

“Kwa upande wa sheria, wengi walitaka elimu kuhusu migogoro ya ardhi na mirathi… hawa wengi kesi zao ziko mahakamani hivyo walitaka elimu ili wajue sheria zinasemaje kuhusu masuala yao,” alisema.

Akizungumzia huduma hizo, Mkurugenzi wa Mradi katika taasisi ya Friedrich Naumann Foundation for Freedom, East Africa kwa Tanzania na Kenya, Veni Swai, alisema, “ changamoto kubwa ni upungufu wa rasilimali yaani muda, watoa huduma na vifaa maana huduma zinatolewa kwa siku mbili kwa kata na hapo, ndipo watu wanaanza kuongezeka na kufanya wahudumu na vifaa vilivyopo kutokidhi idadi ya watu.”

Chanzo: habarileo.co.tz