Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaojifanya Takukuru dawa yenu hii hapa

1bd1993c78d0ab2e66f30235bfe6e35b.png Wanaojifanya Takukuru dawa yenu hii hapa

Fri, 30 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Rukwa, inawasaka watu wanaojipatia fedha kwa njia za kitapeli kwa kujifanya maofisa wake.

Mkuu wa Takukuru wa Mkoa wa Rukwa, Daniel Ntera, alibainisha hayo juzi mjini hapa wakati akitoa taarifa ya utekelezaji kazi katika kipindi cha Aprili hadi Juni, 2021.

Alisema uchunguzi wa awali uliofanywa na maofisa wa taasisi hiyo umebaini kuwa, watu hao wamekuwa wakiwatapeli wafanyabishara wakubwa na watumishi wa umma huku wakijifanya ni maofisa wa Takukuru.

"Nachukua fursa hii kuwaonya wale wote wanaowatapeli wananchi kwa kujifanya ni maofisa wa Takukuru na wale wanaoendelea kujihusisha na vitendo vya rushwa; wenye tabia hiyo nasema waache mara moja, kwani wakikamatwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao," alionya.

Ntera aliwahimiza wafanyabishara, watumishi wa umma na wananchi kwa jumla kutoa taarifa kwa Takukuru au vyom,bo vingine haraka ili kuwatia mbaroni matapeli hao, kabla hawajatekeleza uhalifu wao.

Alisema katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2021, Takukuru itaendelea kudhibiti na kuchambua mifumo kuhusu ubadhirifu wa fedha za serikali katika ugavi wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya umma vinavyotoa huduma za afya ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa iliyopo Sumbawanga.

Alisema uchunguzi wa awali unaoendelea kufanywa na maofisa wa taasisi hiyo umebaini kuwepo kwa baadhi ya watumishi wa afya wanaojihusisha na wizi wa dawa na vifaa tiba.

Alisema taasisi hiyo inazo taarifa za kutosha na orodha ya vituo vyote vya umma vinavyotoa huduma za afya ambapo baadhi ya watumishi wake wanajihusisha na wizi wa dawa na vifaa tiba.

Alisema maofisa wa taasisi hiyo katika kipindi cha Julai hadi Septemba kupitia dawati la uzuiaji rushwa wataendelea kufanya ufuatiliaji wa fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri za wilaya zilizopo mkoani humo.

"Lengo ni kuziba mianya ya rushwa na kudhibiti upoteaji wa fedha za serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo," alisisitiza.

Chanzo: www.habarileo.co.tz