Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaodaiwa kutuma meseji za kitapeli wafikishwa kortini

Wanaodaiwa kutuma meseji za kitapeli wafikishwa kortini

Mon, 9 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakazi watatu wa Sumbawanga mkoani Rukwa  wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shtaka la kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Maria Sasabo kwa nia ya kujipatia fedha.

Washtakiwa hao ni Japhet Mzuri (22), Joseph Richard (24) na Justin Sadoki (25).

Wamesomewa mashtaka leo Jumatatu Machi 9, 2020 na wakili wa Serikali, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi, Rashid Chaungu.

Wakili Simon amedai washtakiwa wanakabiliwa shtaka moja la kusambaza ujumbe wenye lengo la upotoshaji.

Amedai washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo  Januari 18, 2020 katika wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa.

Siku hiyo ya tukio kwa nia ovu, washtakiwa walituma ujumbe mfupi wa maandishi uliosomeka, “chukua namba hii ndio utumie kutuma hiyo pesa 0757 648067 jina litatokea Asha Mwamalekela.”

Pia Soma

Advertisement
Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa walituma ujumbe huo kwa Dk Sasabo kwa nia ya kujipatia fedha wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa.

Washtakiwa wamekana shtaka lao na upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.

Hakimu Chaungu alitoa masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili kutoka Mkoa wa Dar es Salaam watakao saini bondi ya Sh10 milioni kila mmoja.

Pia, wadhamini hao wanatakiwa kuwa na nakala ya kitambulisho cha Taifa pamoja na barua za utambulisho kutoka Serikali ya mtaa.

Washtakiwa hao wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na kupelekwa mahabusu.

Hakimu Chaungu ameahirisha kesi hiyo hadi  Machi 23, 2020.

Chanzo: mwananchi.co.tz